Na Heri Shaaban, JamhuriMedia, Dar es Salaam

MKUU wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo ,ametoa agizo kwa Jeshi la Polisi kupitia Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala, ACP Yustino Mgonja kutumia utaalamu na timu yake kuwakamata mara moja kundi la watu waliofanya mauaji ya mwananchi Mzee Salehe Idd Salehe, nyumbani kwake Mtaa wa Zavala Kata ya Buyuni Mkoani Dar es Salaam.

Mpogolo alisema Mzee Salehe katika Maisha yake amekuwa Mzalendo wa kweli kwa kupigania maeneo ya Wazi ya Serikali mfano Shule, Masoko na Vituo vya Afya yasichukuliwe na genge la Wahalifu wanaouza maeneo hayo ya wazi ya Viwanja vilivyopimwa na Serikali katika Programu ya Viwanja Elfu 20 Kata ya Buyuni kati ya miaka ya 2003/2005.

Mkuu wa Wilaya ametoa agizo hilo kwenye Mkutano wa Wanachi Zavala mara baada kupata taarifa za mauaji ya kifo cha unyama alichofanyiwa Mzee Salehe Idd Salehe hivi karibuni nyumbani kwake majira ya Alfajiri na kundi la watu wahalifu.

“Kamanda RPC wa Ilala nakuagiza tumia vyombo vyako na utaalamu wako na ninahakika unaweza kuakikisha mnawakamata watu wote waliofanya mauaji haya na kufikishwa katika vyombo vya sheria. Kwa kuwa wauaji hawa inaelekea wanao mtandao mkubwa wa kiuhalifu katika eneo letu la Wilaya za kipolisi za Chanika na Ukonga ” alisema Mpogolo.

Mpogolo alisema Jeshi la Polisi chini ya ACP Mgonja lina mfumo na nyenzo imara sana za uchunguzi na ukamataji, hivyo nawaomba wananchi tuwape imani chombo chetu cha Polisi kifanye uchunguzi na kikamate haraka na kuweza kuleta Imani kwa wananchi juu ya Usalama wao na usimamizi wa Sheria.

Aidha Mpogolo alimwagiza Mkurugenzi wa Jiji kupitia Idara ya Mipango Jiji kuendelea kuyatambua na kuyarejesha maeneo yote wazi ya huduma za jamii yaliyolipiwa na kutengwa na serikali. Pia washirikiane na Jeshi la polisi kubaini genge la Wahalifu wa viwanja vya Umma wanao uza kwa watu wasiojua.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo hivi karibuni alifanya ziara kata ya Buyuni eneo la Zavala kuzungumza mkutano na wananchi ambapo kumeleta matumaini na faraja kwa wakazi wa Zavala.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Zavala Faridu Said Rashidi ,amesema katika Mtaa wa Zavala Kata ya Buyuni kwa sasa wananchi wanakaa kwa hofu kubwa kwa kuofia kundi la watu wasio Julikana ambao wamefanya mauaji hayo .

Mwenyekiti Faridu Said Rashid amesema kwa sasa wananchi wanaogopa kuongea kutokana na vitendo hivyo na wengine wamekimbia makazi yao hasa wale waliokuwa wanatetea maeneo ya huduma za jamii yasiuzwe.