Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani
Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani limebaini zaidi ya wanafunzi 500 wa shule za msingi na sekondari waliokuwa wameacha masomo kwa kipindi kirefu, huku likifanikiwa kuwarejesha shuleni wanafunzi 114 kupitia operesheni maalumu ya Polisi Jamii iliyofanyika katika mkoa huo.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake agost 5 ,2026 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase, alisema operesheni hiyo ilibaini wanafunzi 251 wa shule za msingi na 322 wa shule za sekondari ambao hawakuwa wakihudhuria masomo kutokana uelewa mdogo kuhusu umuhimu wa elimu, changamoto za kiuchumi, ukosefu wa mahitaji ya msingi, migogoro ya kifamilia, mimba za utotoni na changamoto za kiafya.
Alifafanua idadi hiyo si ya wanafunzi walioacha shule mwezi Julai pekee, bali ni waliokuwa wameacha masomo katika vipindi tofauti na kukutwa majumbani wakati wa operesheni ya ufuatiliaji.
Morcase alielezea kuwa, kupitia Polisi Kata, walizungumza na wazazi na walezi na kufanikiwa kuwarejesha shuleni wanafunzi 114, akiwemo mwanafunzi mmoja aliyepatiwa mfadhili wa kuendelea na masomo ya Kidato cha Tano katika Shule ya Sekondari Matimbwa wilayani Bagamoyo.
Katika hatua nyingine, alibainisha kwa mwezi Julai 2026, Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani lilifikisha mahakamani kesi 117, ambapo kesi 63 zilisikilizwa na kumalizika, huku watuhumiwa katika kesi 48 wakitiwa hatiani na kuhukumiwa vifungo mbalimbali.
“Miongoni mwa waliohukumiwa ni Salim Musa Masanja (33) wa Kibaha aliyefungwa miaka 20 jela na kuamriwa kulipa fidia ya Sh milioni moja kwa kosa la kumuingizia vidole sehemu za siri mtoto wa miaka sita, pamoja na Samwel Philimon Mang’ombe (29) wa Bagamoyo aliyehukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kosa la kumlawiti mtoto wa miaka 10” alieleza.
Kwa mujibu wa kamanda huyo, operesheni hiyo ni endelevu huku akitoa rai kwa wazazi na walezi kushirikiana na vyombo vya dola kuhakikisha watoto wanapata elimu na kulindwa dhidi ya vitendo vya ukatili.
Morcase aliomba jamii kujenga tabia ya kufichua wale ambao wanafanya vitendo vya ukatili kwa watoto, kuwapa mimba za utotoni,kulawiti na kubaka ili waweze kuchukuliwa hatua kali za kisheria.


