Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Young Africans SC (Yanga), wamefanikiwa kutwaa ubingwa wa NMB Mapinduzi Cup baada ya kuibuka na ushindi wa mikwaju ya penalti 5–4 dhidi ya Azam FC, katika mchezo wa fainali uliochezwa leo Januari 13, 2026, visiwani Zanzibar.
Mchezo huo uliishia kwa sare tasa (0-0) ndani ya dakika 90 za kawaida, hali iliyomlazimu mwamuzi kuongeza dakika 30 za muda wa nyongeza ili kumpata mshindi, lakini hakuna timu iliyofanikiwa kufunga.
Katika dakika ya 115 ya mchezo, golikipa wa Azam FC, Aishi Manula, aliokoa mkwaju wa penalti uliopigwa na Pacôme Zouzoua, hata hivyo Azam FC walishindwa kuibuka na ushindi kwenye mikwaju ya penalti.
Licha ya Azam FC kucheza pungufu kuanzia dakika ya 74 baada ya mmoja wa wachezaji wao kuoneshwa kadi nyekundu, walionyesha upinzani mkubwa na kucheza kwa nidhamu kubwa dhidi ya Yanga.
Kwa ushindi huo, Yanga wametwaa ubingwa wa NMB Mapinduzi Cup kwa mara ya tatu, huku bingwa wa michuano hiyo akipata zawadi ya Shilingi milioni 150 pamoja na kombe, huku mshindi wa pili akipata milioni 100.

