Na Mwandishi Wetu, Morogoro
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano ya Kazi, Deus Sangu, ameridhishwa na maendeleo makubwa yaliyofikiwa katika mradi wa Kiwanda cha Sukari Mkulazi, ndani ya muda mfupi kiwanda hicho kitaanza kujiendesha kwa faida, hatua inayoendana na maono ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuendeleza miradi ya kimkakati nchini.
Sangu aliyasema hayo wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua maendeleo ya mradi huo, akiwa ameambatana na viongozi wa taasisi wabia wa kiwanda hicho akiwemo Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba, pamoja na Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Magereza, ACP Dominic Kazmil. Kiwanda hicho kinamilikiwa kwa ubia na NSSF pamoja na Jeshi la Magereza kupitia Shirika lake la uzalishaji mali (SHIMA).
“Niwapongeze wawekezaji wa mradi huu, NSSF na Jeshi la Magereza, kama Serikali, tunashukuru kwa mchango mkubwa wa mradi huu katika kuzalisha ajira, jambo ambalo ni mwelekeo wa Serikali ,” alisema Sangu.
Alibainisha ,mradi huo tayari umeanza kuleta tija kwa Taifa na jamii kwa ujumla, ambapo hadi sasa umeweza kuzalisha ajira za moja kwa moja 1,920 na ajira zisizo za moja kwa moja takribani 8,000, ndani ya muda mfupi tangu ulipoanza kutekelezwa.
Sangu alieleza kiwanda kitachochea uchumi wa Taifa, kuongeza mapato ya kodi, kuzalisha ajira kwa Watanzania na kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na jamii.
“Kiwanda hiki ni cha kimkakati na kinatekeleza maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuacha tabasamu kwa Watanzania, kwani tayari kimeanza kuleta mabadiliko chanya kwa Taifa na jamii kwa ujumla,” anaeleza.
Aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara zinazounganisha mashamba ya wakulima wadogo wa miwa na kiwanda, hatua itakayorahisisha usafirishaji wa miwa na kuongeza uzalishaji.
Aliahidi kuufuatilia mradi huo kwa karibu ili kuhakikisha unatimiza lengo la kupunguza nakisi ya sukari nchini, akieleza kuwa katika mwaka wa uzalishaji 2027/2028, kiwanda kinatarajiwa kuzalisha tani 50,000 za sukari.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni Hodhi ya Mkulazi, Dkt. Hildelitha Msita, aliishukuru Serikali kwa kuwekeza katika miradi inayogusa maisha ya wananchi na kukuza uchumi wa Taifa, huku akiahidi kuendelea kuusimamia mradi huo kwa weledi.
Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba, aliishukuru Serikali kwa usimamizi mzuri wa mradi huo, akibainisha kuwa kama wabia watahakikisha kiwanda kinasimamiwa ipasavyo ili kufikia malengo ya mradi na kuleta faida endelevu kwa wanachama na Taifa kwa ujumla.
ACP Dominic Kazmil alisema ushirikiano uliopo kati ya NSSF na Jeshi la Magereza umechangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya mradi huo.
Diwani wa Kata ya Mkulazi, Edward William, aliishukuru Serikali kwa uwekezaji wa kiwanda hicho, akisema kimeleta manufaa makubwa kwa wananchi wa kata hiyo kupitia ajira, fursa za kiuchumi na uboreshaji wa huduma za kijamii.









