Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma

Zaidi ya viongozi 31,000 wa sekta ya elimu nchini wamejengewa uwezo kupitia mafunzo ya uongozi na usimamizi yanayotolewa na Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM), huku zaidi ya Sh. bilioni 16 zikiwekezwa katika kuimarisha uongozi wa shule za msingi na awali kupitia Mradi wa BOOST.

Hatua hiyo imeelezwa kuwa ni sehemu ya mageuzi makubwa ya Serikali ya awamu ya sita yanayolenga kuhakikisha uwekezaji mkubwa unaofanyika katika miundombinu ya elimu, maboresho ya mitaala na matumizi ya teknolojia unasimamiwa na viongozi wenye ujuzi, weledi na uwajibikaji.

Akizungumza na waandishi wa habari Leo Agosti 6,2026 Dodoma, Kaimu Mtendaji Mkuu wa ADEM Dkt. Maulid Maulid amesema taasisi hiyo imeendelea kuwa mhimili muhimu wa utekelezaji wa sera za elimu kwa kuwajengea uwezo viongozi wa shule, maafisa elimu, wathibiti ubora wa shule na watendaji wengine ili kuongeza ufanisi wa usimamizi wa elimu nchini.

Amesema tangu kuanzishwa kwake mwaka 2001, ADEM imekuwa ikiandaa mafunzo ya muda mrefu na muda mfupi, kufanya tafiti na kutoa ushauri wa kitaalamu unaosaidia kuboresha mfumo wa elimu na kuongeza ubora wa utoaji wa huduma katika shule na taasisi za elimu.

Ameongeza kuwa, wahitimu 8,599 wamekamilisha Stashahada ya Uongozi, Usimamizi na Utawala katika Elimu (DELMA) kati ya mwaka 2002 na 2025, huku wahitimu 2,263 wakikamilisha Stashahada ya Uthibiti Ubora wa Shule (DSQA) kuanzia mwaka 2016 hadi 2025.

Aidha, katika mwaka wa masomo 2025/2026, ADEM ilidahili wanafunzi 2,016, wakiwemo 1,634 wa programu ya DELMA na 382 wa programu ya DSQA.

Katika kuimarisha uongozi wa shule kupitia Mradi wa BOOST, amesema ADEM imepokea zaidi ya Sh. bilioni 16.16 kwa kipindi cha miaka mitano, fedha zilizowezesha kutoa mafunzo kwa walimu wakuu 17,817, waratibu elimu kata 3,907, pamoja na maafisa elimu wa mikoa na wilaya 208.

Mbali na mafunzo hayo, ameeleza kuwa fedha hizo zimetumika kuandaa na kuchapisha miongozo muhimu ya usimamizi wa shule ikiwemo School Management Manual na LGA’s Education Good Governance Manual, ambayo imeimarisha utawala bora katika shule na mamlaka za serikali za mitaa.

Katika hatua nyingine, Dkt. Maulid amesema ADEM imeingia ubia na mashirika mbalimbali ya kimataifa, ikiwemo VVOB-Education for Development, kutekeleza programu ya miaka mitano ya kuwajengea uwezo wakuu wa shule za sekondari, manaibu wao, maafisa elimu wa mikoa na wilaya pamoja na waratibu elimu kata.

Kupitia programu hiyo, viongozi 608 tayari wamepatiwa mafunzo, huku lengo likiwa kuwafikia zaidi ya wakuu wa shule 12,000 na kuchangia kuboresha ujifunzaji wa wanafunzi zaidi ya milioni 2.8 ifikapo mwaka 2030.

“ADEM pia imeendelea kufanya tafiti zinazolenga kuboresha uongozi na usimamizi wa shule, matumizi ya jumuiya za kujifunza, ujumuishaji wa wanafunzi wenye mahitaji maalumu na matumizi ya teknolojia katika usimamizi wa elimu,”amesema.

Amesema Matokeo ya tafiti hizo yamechangia upatikanaji wa fedha za utafiti kwa vyuo vikuu mbalimbali nchini, ikiwemo UDOM, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Open University of Tanzania, DUCE, MUCE, St. John’s University, University of Arusha pamoja na ADEM yenyewe.

Katika kuimarisha ushirikiano wa kimataifa, Mkurugenzi huyo ameeleza ADEM imeendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali zikiwemo UNESCO, World Bank, VVOB, African Centre for School Leadership (ACSL), Plan International, CAMFED na IRC, hatua inayolenga kuboresha mafunzo, tafiti na matumizi ya teknolojia katika uongozi wa elimu.

Kwa upande wa miundombinu, amesema Wakala unaendelea na ujenzi wa jengo la mafunzo katika Kampasi ya Mbeya pamoja na maandalizi ya ujenzi wa kumbi changamani katika Kampasi ya Bagamoyo utakaogharimu takribani Sh. bilioni 14, huku maandalizi ya ujenzi wa kumbi za mihadhara katika Kampasi ya Mwanza yakiendelea.

“Kwa mwaka wa fedha 2026/2027, ADEM imepanga kuongeza udahili wa wanafunzi kutoka 2,016 hadi 3,500, kuongeza washiriki wa mafunzo ya muda mfupi kutoka 5,220 hadi 7,521, kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika mafunzo na kupanua ushirikiano wa kimataifa ili kuiwezesha Tanzania kuwa kitovu cha mafunzo ya uongozi wa elimu katika Afrika Mashariki na ukanda wa SADC,”amesema.

Pamoja na hayo ADEM imesema itaendelea kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Ofisi ya Rais-TAMISEMI kuhakikisha viongozi wa elimu wanakuwa na uwezo wa kusimamia rasilimali za umma kwa ufanisi, kuongeza uwajibikaji na kuboresha matokeo ya elimu, sambamba na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.