Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) imesema itaendelea kutumia sekta ya michezo ili kujenga mahusiano ya undugu, ujamaa, umoja na mshikamano ili kuenzi misingi ya Muungano.

Rai hiyo imetolewa leo Ijumaa (Januari 23, 2026) na Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Dkt. Richard Muyungi wakati wa ziara yake ya kutembelea kambi ya timu ya Netiboli ya Ofisi hiyo inayoshiriki mashindano ya Ligi ya Muungano ya netiboli inayoendelea katika Uwanja wa Amani Complex, Zanzibar.

Dkt. Muyungi amesema michezo ni sekta muhimu inayotumika katika kujenga mashirikiano na uhusiano katika jamii na hivyo Ofisi yake itaendeleza jitihada mbalimbali katika kuhakikisha michezo itakuwa sehemu muhimu katika kuimarisha Muungano.

“Nia na malengo ya waasisi wetu wakati kuanzia Muungano ni  kuhakikisha wanatumia fursa mbalimbali ikiwemo michezo ili kuweza kujenga mahusiano ya undugu, familia na fursa nyingine za kijamii na kiuchumi” amesema Dkt. Muyungi.

Ameeleza kupitia sekta ya michezo hususani mashindano ya Ligi ya Netiboli, Ofisi hiyo imeweza kutangaza vyema Muungano ambapo wachezaji wa timu wameweza kucheza kwa juhudi kubwa na kuibuka kwa matokeo ya ushindi katika michezo yake.

Aidha katika ziara hiyo Dkt. Muyungi pia alikabidhi zawadi ya pesa taslimu Shilingi 500,000/- kwa kila mchezaji wa timu hiyo na bench la ufundi ikiwa ni sehemu ya motisha ya kuwaongezea morali ya kupata matokeo ya ushindi katika michezo yake iliyosalia.

“Nimetoa zawadi hii ya pesa kama motisha kwenu kwa ajili ya kufanya vizuri zaidi, niseme tu yajayo yanafurahisha…tuongeze juhudi katika michezo iliyosalia ili tuweze kuchukua ubngwa wa mashindano haya” amesema Dkt. Muyungi.

Kwa upande wake Kocha wa Timu wa hiyo, Bw. Mafuru Buriro ameishukuru Menejimenti ya Ofisi hiyo  kwa kuwawezesha kupata mahitaji yote ya muhimu hatua iliyowezesha kuwa na kambi nzuri iliyojiandaa vyema kwa ajili ya mashindano hayo.

“Tunamshukuru sana Katibu Mkuu kwa kuwa karibu na timu tangu mwanzo wa mashindano haya kwani hiyo ndiyo siri ya matokeo haya mazuri katika michezo yetu tuliyocheza” amesema Buriro.

Amesema timu hiyo imecheza jumla ya michezo 10 ambapo imeshinda michezo 9 na kupoteza mchezo mmoja dhidi ya timu ya Kikosi cha Valantia Zanzibar (KVZ) ambao ni mabingwa watetezi wa mashindano hayo.

Kwa upande Katibu wa Klabu ya Michezo Ofisi ya Makamu wa Rais, Bw. Marwa Nyaisawa amesema mashindano ya Ligi ya Muungano ya Netiboli ni moja ya mashindano mahsusi yaliyoionesha jamii utayari wa Ofisi hiyo katika kuonesha ushindani wa michezo mbalimbali.

Naye mchezaji wa timu hiyo, Bi. Habiba Mhina ameishukuru Menejimenti ya Ofisi hiyo kwa kutoa nafasi kwa watumishi wanawake kushiriki mashindano hayo kwani kwani mbali na kuimarisha afya zao pia michezo hiyo pia imewakutanisha na watumishi wenzao.

Mashindano ya Ligi ya Muungano ya Netiboli mwaka 2026, yalishirikisha jumla 11 ikiwemo timu sita (06) kutoka Tanzania Bara na timu tano (05) kutoka Zanzibar. Hadi kufikia sasa Timu ya Netiboli ya Ofisi ya Makamu wa Rais inashika nafasi ya pili baada ya kushinda michezo yake 09 na kupoteza mmoja.

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Richard Muyungi akiwasili katika Uwanja wa Amani Complex, Zanzibar kuzungumza na wachezaji wa timu ya netiboli ya Ofisi hiyo inayoshiriki mashindano ya Ligi ya Muungano ya Netiboli. Anayempokea ni Mkurugenzi wa Muungano Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Juma Mohammed Salum.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Richard Muyungi akisalimiana na wachezaji watimu ya Netiboli ya Ofisi hiyo wanayoshiriki mashindano ya Ligi ya Muungano ya Netiboli inayoendelea katika Uwanja wa Amani Complex, Zanzibar muda mfupi baada ya kuwasili katika kambi ya timu kwa ajili ya kuwapongeza kwa matokeo mazuri katika mashindano hayo.
Mkurugenzi wa Muungano Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Juma Mohammed Salum akizungumza jambo wakati wa ziara ya Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Richard Muyungi alipotembelea kambi ya timu ya netiboli ya ofisi hiyo inayoshiriki Ligi ya Muungano ya Netiboli kwa ajili ya kuwapongeza kwa matokeo mazuri katika mashindano hayo.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais akimkabidhi zawadi ya pesa taslimu mchezaji wa timu ya mpira wa pete (netiboli) ya Ofisi hiyo, Bi. Habiba Mhina wakati alipotembelea kambi ya timu hiyo inayoendelea na mashindano ya Ligi ya Muungano ya Netiboli kwa ajili ya kuwapongeza kwa matokeo mazuri katika mashindano hayo.
Kikosi cha timu ya mpira wa pete cha Ofisi ya Makamu wa Rais wakiwa katika picha ya pamoja muda mfupi kabla ya kuanza kwa mchezo baina yao na timu ya Zimamoto leo Ijumaa Januari 23, 2026 katika mwendelezo wa mashindano ya Ligi ya Muungano ya Netiboli yanayoendelea katika Uwanja wa Amani Complex, Zanzibar.
Wachezaji wa Timu ya mpira wa pete ya Ofisi ya Makamu wa Rais wakisikiliza maelekezo ya kocha wa timu hiyo, Bw. Mafuru Buriro wakati wa muda wa mapumziko katika mchezo baina yao na Timu ya Zimamoto leo Ijumaa Januari 23, 2026 ikiwa ni mfululizo wa mashindano ya Ligi ya Muungano ya Netiboli yanayoendelea katika Uwanja wa Amani Complex Zanzibar.