London, Uingereza — Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo (Mb.), amewahakikishia wawekezaji wa Uingereza kwamba Tanzania ni nchi salama, yenye uthabiti wa kisiasa, na inayotekeleza maboresho endelevu ya mazingira bora na rafiki kwa uwekezaji.

Waziri Mkumbo alisema hayo akizungumza katika Mkutano wa Uwekezaji kati ya Tanzania na Uingereza ulioandaliwa na taasisi ya Clyde & Co wakati wa ziara yake ya kikazi inayoendelea nchini humo.

Katika hotuba yake, Waziri Mkumbo alisema Tanzania inaanza safari ya kuelekea Dira ya Taifa 2050 ikiwa katika nafasi nzuri, ikichochewa na uthabiti wa uchumi, utulivu wa kisiasa na mageuzi yanayoendelea kuboresha mazingira ya biashara.

Waziri Mkumbo alieleza kuwa uchumi wa Tanzania umeendelea kuimarika baada ya janga la UVIKO-19, ambapo kasi ya ukuaji imeongezeka kutoka asilimia 4.7 mwaka 2022 hadi asilimia 5.9 mwaka 2025, huku ikitarajiwa kufikia asilimia 6.3 mwaka 2026. Aliongeza kuwa kiwango cha mfumuko wa bei kimeendelea kubaki chini ya asilimia 5 kwa zaidi ya muongo mmoja, hali inayotoa uhakika wa utulivu wa kiuchumi.

Akizungumzia mazingira ya uwekezaji, Waziri Mkumbo alibainisha kuwa Serikali inaendelea kuimarisha amani na usalama, kutekeleza maboresho endelevu ya mfumo wa kodi na udhibiti, kwa lengo la kuongeza uwazi, utabiri wa sera, na ufanisi wa utoaji huduma kwa wawekezaji. Alisisitiza kuwa Kituo cha Uwekezaji cha Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi (TISEZA) kilifanyiwa maboresho ya kimuundo kutoka taasisi mbili kuwa moja ili kuongeza ufanisi na kutoa huduma bora kwa wawekezaji.

Waziri Mkumbo pia aliwasilisha dira pana ya fursa za uwekezaji nchini, akieleza kuwa Tanzania imebarikiwa ardhi kubwa yenye rutuba (zaidi ya hekta milioni 44), rasilimali nyingi za madini na nishati, pamoja na jiografia ya kimkakati inayoiunganisha Afrika Mashariki, Kati na Kusini kupitia bandari, reli, barabara na anga. Alisisitiza kuwa Tanzania ina madini 22 ya kimkakati yanayohitajika katika ajenda ya mpito wa nishati duniani.

Akirejea uhusiano wa Tanzania na Uingereza, Waziri Mkumbo alisema nchi hizo mbili zina zaidi ya miongo sita ya ushirikiano wa kiuchumi wenye tija, ambapo biashara ya pande mbili imefikia pauni milioni 650, huku uwekezaji wa Uingereza wa takribani pauni bilioni 4.89 ukiwa umezalisha zaidi ya ajira 131,000 nchini Tanzania.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Clyde & Co, Bw. Michael Clayton, aliipongeza Tanzania kwa mwelekeo wake wa mageuzi na kusisitiza kuwa majukwaa kama hayo ni muhimu katika kujenga imani, kuondoa sintofahamu, na kuimarisha ushirikiano wa muda mrefu kati ya Serikali na wawekezaji wa kimataifa.

Akihitimisha hotuba yake, Waziri Mkumbo aliwaalika wawekezaji wa Uingereza kuwa washirika wa karibu wa Tanzania katika kutafsiri Dira ya 2050 kuwa uhalisia, akisisitiza: “Tuko wazi kwa biashara. Tunafanya mageuzi. Tunakua. Na tuko tayari kushirikiana.”