* Kuongeza Ushirikiano wa Kidiplomasia na Vatican katika masuala ya amani, mazungumzo na maendeleo ya kijamii

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jana ilithibitisha upya urafiki wake wa muda mrefu na Vatican (Holy See), baada ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Mahmoud Thabit Kombo (Mbunge), kupokelewa na Baba Mtakatifu Papa Leo XIV katika mazungumzo maalum mjini Vatican.

Katika mazungumzo hayo, Waziri Kombo aliwasilisha salamu za heri pamoja na ujumbe maalum kutoka kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Alieleza shukrani za Serikali ya Tanzania kwa msisitizo wa mara kwa mara wa Papa kuhusu amani, mazungumzo na heshima ya utu wa binadamu—maadili ambayo Tanzania inayatambua kuwa msingi muhimu wa mfumo wa kimataifa ulio imara, wa haki na wenye huruma.

Waziri Kombo alibainisha kuwa kwa miaka mingi Tanzania imeendelea kupata nguvu kupitia uhusiano wake na Vatican, ushirikiano unaojengwa juu ya heshima ya pande zote, huduma kwa jamii na imani ya pamoja katika utu wa binadamu. Alisema kuwa ushirikiano huo unaonekana wazi katika maisha ya kila siku ya Watanzania kupitia mchango wa Kanisa Katoliki katika sekta za elimu, afya na kuwasaidia walio pembezoni, sambamba na juhudi za maendeleo ya taifa.

Serikali ilisisitiza kuthamini kwa kina mchango wa taasisi za Kanisa Katoliki zinazoendelea kusaidia maendeleo ya elimu, afya na ustawi wa jamii nchini Tanzania, pamoja na fursa zinazotolewa kwa wanafunzi wa Kitanzania kusoma katika taasisi za Kipapa. Waziri alisema kuwa mahusiano hayo ni muhimu katika kujenga ujuzi, maadili na uhusiano wa kudumu kati ya watu wa mataifa hayo mawili.

Waziri Kombo pia alithibitisha kutambua kwa Serikali mchango muhimu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) katika maisha ya kijamii na kiraia ya taifa. Alisisitiza dhamira ya Tanzania ya kuendeleza ushirikiano wa wazi, wa kuheshimiana na wenye kujenga na Kanisa katika ngazi zote, kwa kuzingatia mazungumzo, busara na kulinda maslahi ya pamoja ya taifa.

Aidha, alisema Tanzania inathamini uongozi wa kimaadili wa Kanisa Katoliki katika kuhamasisha umoja, huruma na matumaini, hususan katika nyakati za mabadiliko ya kisiasa.

Serikali ilikaribisha mchango unaoendelea wa Kanisa katika kuimarisha mshikamano wa kitaifa, ikieleza kuwa ujumbe unaohimiza umoja, mazungumzo na kujizuia unapokelewa kwa uzito na kuimarisha nafasi ya Kanisa kama nguzo ya amani na maadili ndani ya jamii ya Kitanzania.

Akizungumzia vurugu zilizotokea katika baadhi ya maeneo ya nchi baada ya Uchaguzi Mkuu wa tarehe 29 Oktoba 2025, Waziri Kombo alisisitiza dhamira ya Serikali ya kurejesha utulivu na kurejea katika hali ya kawaida. Alieleza kuwa Rais Samia ameongoza juhudi za kitaifa katika kujenga upya imani na umoja, ikiwemo kuanzisha mchakato huru wa tathmini unaoongozwa na Jaji mstaafu anayeheshimika, kwa lengo la kubaini ukweli kwa uwazi, kujifunza na kuzuia matukio kama hayo yasijirudie.

Serikali ilisisitiza tena dhamira ya Rais ya kuendeleza mazungumzo jumuishi na vyama vya siasa, wazee, vijana, viongozi wa dini na asasi za kiraia, kwa kuongozwa na falsafa yake ya 4R: Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Ujenzi Upya. Katika muktadha huo, Waziri aliomba Baba Mtakatifu kuendelea kuliombea taifa hilo ili mchakato huo ufaulu, pamoja na kuombea amani, umoja na ustawi wa Tanzania na wananchi wake.

Baba Mtakatifu Papa Leo XIV alikaribisha ombi hilo na kueleza utayari wake wa kuliombea taifa la Tanzania amani, umoja na maridhiano. Alikumbuka kwa furaha miaka yake ya awali alipokuwa Tanzania, akishiriki kumbukumbu za huduma za kichungaji katika jumuiya za kimisionari huko Songea, Morogoro, Arusha na Dar es Salaam. Alisema kuwa uzoefu huo ulimwacha na kumbukumbu za kudumu na umeendelea kuimarisha uhusiano wake wa karibu na Tanzania na watu wake.

Mbali na mazungumzo na Papa, Waziri Kombo na ujumbe wake walifanya pia mazungumzo rasmi na Askofu Mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu wa Vatican anayesimamia Mahusiano na Nchi na Mashirika ya Kimataifa, kwa lengo la kuimarisha zaidi uhusiano wa kidiplomasia na kuongeza ushirikiano wa kimfumo kati ya Tanzania na Vatican.

Katika mazungumzo hayo, Waziri Kombo aliipokea ombi la Vatican kwa Tanzania kuanzisha uwakilishi wa kidiplomasia wa kudumu mjini Vatican. Kwa sasa Tanzania inawakilishwa na Balozi asiye mkazi mwenye makazi yake Berlin, Mheshimiwa Hassan Iddi Mwamweta, ambaye alihudhuria vikao hivyo.

Serikali ilieleza kuwa hatua hiyo inayopendekezwa ni ya vitendo katika kuimarisha ushirikiano wa pande mbili na kudumisha mawasiliano ya mara kwa mara kuhusu vipaumbele vya pamoja.

Ujumbe wa Tanzania uliongozwa na Mheshimiwa Mahmoud Thabit Kombo (Mbunge) na ulijumuisha Mheshimiwa Palamagamba Kabudi, Waziri wa Nchi; Mheshimiwa Hassan Iddi Mwamweta, Balozi asiye mkazi kwa Vatican mwenye makazi Berlin; pamoja na Balozi Noel E. Kaganda, Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Serikali ilieleza kuwa ziara hiyo ya Vatican inaakisi mwelekeo wa diplomasia ya Tanzania kwa mwaka 2026, kama ulivyoainishwa na Rais Samia katika hotuba yake kwa jumuiya ya kidiplomasia katikati ya Januari, akieleza kuwa Tanzania ni “isiyofungamana na upande wowote lakini inayoshirikiana na wote,” ikifuata mkakati wa uhalisia wa kidiplomasia kwa kushirikiana na wadau wote kwa nia njema, huku ikisukuma mbele umoja wa kitaifa na ustawi wa pamoja.