Huku juhudi za kidiplomasia zikiendelea kuzuia mzozo mpana Mashariki ya Kati, Saudi Arabia, mataifa ya Ghuba na Israel zinaweka mbele maslahi yao wakati mvutano kati ya Marekani na Iran ukiendelea kuongezeka.

Katika wiki iliyopita, hali ya wasiwasi kuhusu uwezekano wa Marekani kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Iran iliendelea kuathiri maamuzi ya kimkakati katika eneo lote.

Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu, washirika wa karibu wa Marekani ambao pia wana mahusiano na Tehran, zilisema hazingeruhusu anga zao kutumiwa kwa shambulio lolote, bila kujali linatoka wapi.

Waziri wa mambo ya nje wa Misri, Badr Abdelatty — ambaye nchi yake imeanza kurejesha mahusiano na Iran lakini bado haijafikia ngazi kamili ya kidiplomasia — alizungumza na mwenzake wa Iran Abbas Araghchi pamoja na mjumbe wa Marekani kwa Mashariki ya Kati Steve Witkoff ili “kufanya kazi kuelekea kupatikana kwa utulivu, kwa lengo la kuepusha eneo hilo kutumbukia katika mzunguko mpya wa misukosuko.”

Wakati huohuo, manowari ya kivita ya Marekani inayotumia nishati ya nyuklia, USS Abraham Lincoln, pamoja na takriban meli 10 za kivita zenye makombora ya kuongozwa, zenye uwezo wa kushambulia kutoka baharini, zilifika katika eneo hilo, kwa mujibu wa tovuti ya ufuatiliaji wa usafirishaji wa majini, MarineTraffic.

Shirika la habari la serikali ya Iran, Press TV, lilitangaza kuwa kuanzia mwanzo wa wiki hii, vikosi vya majini vya Walinzi wa Mapinduzi ya Iran vitaanza mazoezi ya kijeshi ya kutumia risasi halisi katika maji hayo hayo — Mlango wa Hormuz — unaounganisha Saudi Arabia, Iran, Iraq na Umoja wa Falme za Kiarabu na Ghuba ya Oman pamoja na Bahari ya Arabuni.

Wakati huo huo, ujumbe wa Iran katika Umoja wa Mataifa uliandika kwenye X kwamba “Iran iko tayari kwa mazungumzo yanayozingatia heshima na maslahi ya pande zote — LAKINI IKISUKUMWA, ITAJILINDA NA KUJIBU KWA NJIA AMBAYO HAIJAWAHI KUTOKEA.”

Sambamba na hilo, Ali Shamkhani, mshauri mkuu wa kiongozi wa juu wa Iran, aliandika kwenye X kwamba dhana ya “shambulio dogo” ni ndoto tu.