Ujue kwa Undani Ugonjwa Uliomuua Agness Maogange

Taarifa tulizopokea leo ni kuwa aliyekuwa video vixen Agnes Gerald maarufu Masogange amefariki dunia mchana wa leo. Wakili wa mlimbwende huyo, Roben Simwanza amethibitisha kutokea kwa kifo hicho majira ya saa 10 jioni leo Ijumaa April 20, 2018. Semwanza amesema kuwa Masogange alikuwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Mama Ngoma iliyoko Mwenge, Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam kutokana na kusumbuliwa na maradhi ya ‘pneumonia’. “Nimeshtushwa na habari hii. nilipokea simu nikitaarifiwa kuhusu kifo chake majira ya saa 10 za jioni,” alisema Wakili Semwanga. Kutokana na kifo hicho kuwa cha kusikitisha na cha ghafla, wasanii na watu engine mbalimbali wameonyesha kuumizwa na akiwemo msanii Steve Nyerere.

Je ugonjwa wa pnemuonia ni nini?

Pneumonia ni maambukizi katika viriba ya hewa katika pafu moja au mapafu yote. Viriba hivi vya hewa huweza kujaa maji au usaha na kusababisha mgonjwa kukohoa, homa kali na kupumua kwa shida. Pneumonia hubebwa na bakteria, virusi au fangasi.

Pneumonia inaweza kuwa ya kawaida na ikapona lakini wakati mwingine huwa ni tishio kwa uhai na huweza kuleta kifo kama ambavyo tumeona kwa ndugu yetu Agnes (Masogange). Ugonjwa huu mara nyingi huwapata watoto wadogo au watu wenye umri zaidi ya miaka 65 lakini pia huweza kuwapata watu ambao mfumo wao wa kinga mwilini umeshambuliwa na magonjwa nyemelezi.

Dalili

Dalili ziko mbalimbali na hutofautiana toka dalili za awali hadi zile ambazo ni kubwa zaidi. Tofauti ya dalili wakati mwingine haisababishwi na muda tu ambao mgonjwa ameugua bali pia nini kimesababisha, umri wa mgonjwa na kinga yake ya mwili kwa ujumla. Dalili za kati kawaida huwa kama za mafua au kikohozi lakini hudumu kwa muda mrefu.

Dalili huweza kuwa:

  • Maumivu ya kifua unapokohoa au kuhema.
  • Kuchanganywa mambo (mental Confusion). Hii mara nyingi hutokea kwa watu ambao wana umri zaidi ya miaka 65.
  • Kikohozi kizito
  • Uchovu usioisha
  • Homa, kutoka jasho na kutetemeka mwili.
  • Joto la mwili kushuka kuliko kawaida (hii pia hutokea kwa watu ambao wana umri zaidi ya miaka 65 au wana kinga pungufu ya mwili)
  • Kichefuchefu, kutapika na kuharisha.
  • Kuishiwa pumzi.

Watoto wachanga wanaweza wasionyeshe dalili zozote za maambukizi. Au wanaweza kutapika na kuwa na homa na kukohoa, na kuwa hawajatulia, kuishiwa nguvu na kushindwa kupumua au kula.

Muda gani umuone daktari?

Muone daktari mara moja unapoona una shida ya kupumua, maumivu ya kifua, homa isiyoisha (Nyuzi joto za mwili 39 za Celcius au zaidi) au kukohoa kusikokoma.

Ni vyema zaidi pia kwa watu wenye hali hizo hapo juu kumuona daktari hasa:

  • Kama wana umri zaidi ya miaka 65
  • Watoto wadogo wa miaka miwili kushuka chini.
  • Watu wenye matatizo mengine ya afya na mfumo wa kinga ambao ni dhaifu
  • Watu ambao wana saratani na wanapokea matibabu ya mionzi au dawa nyingine ambazo huweza kuleta tatizo kwa mfumo wa kinga mwilini.

Husababishwa na nini?

Sababu kubwa huwa ni bakteria ambao wako katika hewa tunayovuta. Kawaida kila siku unavuta bakteria hawa lakini mwili unajilinda ili wasilete tatizo katika mapafu yako. Lakini wakati mwingine vimelea hivi huizidi nguvu kinga yako ya mwili, wakati mwingine mwingine hata kama afya yako ni nzuri.

Pneumonia huwekwa katika makundi kulingana na vimelea (germs) ambao wameisababisha. Inaweza kuwa Pneumonia ya Bakteria, Virusi au Fangasi. Hizo za hayo makundi matatu kwa pamoja pia huitwa pneumonia inayopatikana toka kwenye jamii (community acquired pneumonia).

Aina nyingine ni pneumonia inayopatika toka hospitali (hospital acquired pneumonia). Hii hupatikana wakati mwingine mtu anapokuwa amelazwa hospitali. Hii wakati mwingine ni ngumu kupona kwa sababu unaambukizwa toka kwa watu ambao tayari wako katika matibabu na bakteria wake ni ngumu kumalizika kwa dawa (anti-biotics).

Jilinde

  • Pata chanjo
  • Epuka sigara na uvutaji tumbaku wa ujumla
  • Tunza mfumo wako wa kinga kwa kuzingatia kanuni za afya
  • Tunza usafi
  • Watoto wapate chanjo

 

Source: Swahili Times