Taarifa zilizotolewa na idara ya ujasusi ya Ukraine zinaonyesha kuwa Urusi inajiandaa kufanya mashambulizi zaidi na kuilenga miundombinu ya nishati.

Hayo yameelezwa na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky na kuongeza kuwa mashambulizi yoyote yatafanya iwe vigumu kufikia makubaliano ya kukomesha vita hivyo vya karibu miaka minne. Zelensky amesema ni muhimu kuhakikisha kwamba mifumo yote ya ulinzi wa anga imewekwa katika hali ya tahadhari.

Wajumbe wa Ukraine, Urusi na Marekani wanatarajiwa kukutana Jumanne mjini Geneva nchini Uswisi kushiriki duru ya tatu ya mazungumzo yanayosimamiwa na Marekani na ambayo kwa mara ya kwanza yatajadili kwa kina kuhusu suala la vita na hatima ya maeneo ya Ukraine yanayokaliwa na Urusi, hasa jimbo la Donbas ambalo Moscow inataka Ukraine iliachie.