Iran imetangaza Jumanne kufungwa kwa muda kwa Mlango Bahari wa Hormuz, kwa ajili ya kuendeleza luteka ya kijeshi yenye nia ya kuonyesha uwezo wa Jamhuri hiyo ya Kiislamu.
Hatua hiyo imechukuliwa huku wapatanishi wa Tehran wakiwa wamekamilisha mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja na Marekani kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran huko mjini Geneva, Uswisi.
Tangu Marekani kuanzisha vitisho vya kuishambulia Iran, hii ni mara ya kwanza kwa Tehran kutangaza kufungwa kwa Mlango Bahari wa Hormuz ambayo ni njia hii muhimu ya kimataifa inatumiwa kusafirisha asilimia 20 ya mafuta yanayotumiwa kote duniani.
Wakati Marekani ikiongeza uwepo wa vikosi vyake vya kijeshi katika eneo la Mashariki ya Kati, Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei ameonya kwamba hata jeshi lenye nguvu zaidi duniani linaweza wakati mwingine kupata pigo kubwa kiasi cha kushindwa kusimama tena.


