Mahakama ya Tunisia imemhukumu mbunge mmoja kifungo cha miezi minane jela kutokana na kuchapisha mitandao ya kijamii akimkejeli Rais Kais Saied kufuatia mafuriko yaliyosababisha vifo vya hivi karibuni.
Ahmed Saidani alikamatwa mapema mwezi huu baada ya kuchapisha kwenye mitandao ya kijamii kuhusu ziara za Saied katika maeneo yaliyokumbwa na mafuriko, akimtaja kuwa “kamanda mkuu wa usafi wa mazingira na mifereji ya maji ya mvua”.
Alifungwa gerezani siku ya Alhamisi kwa mashtaka ya kuwatusi wengine kupitia mitandao ya mawasiliano, afisa wa mahakama alisema.
Wakili wa Saidani, Houssem Eddine Ben Attia, aliliambia shirika la habari la AFP kwamba mteja wake anafunguliwa mashitaka chini ya sheria ya mawasiliano dhidi ya “kuwadhuru wengine kupitia mitandao ya kijamii”, kosa ambalo linaweza kuadhibiwa hadi miaka miwili jela.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu yamekosoa kile wanachoeleza kuwa ni kukithiri kwa ukandamizaji wa Saied dhidi ya wapinzani tangu aliposimamisha bunge la Tunisia mwaka 2021 na kuanza kutawala kwa amri.
Saidani, ambaye aliwahi kuwa mfuasi wa uimarishaji wa mamlaka ya Saied na kukamatwa kwa viongozi wa upinzani, hivi karibuni amegeuka kuwa mkosoaji mkubwa wa rais.
Katika chapisho lake la Facebook, mbunge huyo alimkejeli rais kwa “kuchukua hobby ya kupiga picha na maskini ” wakati akizuru maeneo yaliyofurika katika mji mkuu, Tunis na maeneo mengine ya nchi.

