Asema Rais Dkt. Samia amewapa urithi watoto wa kitanzania wa kupata elimu_
▪️Apongeza utekelezaji wa mradi huo kwa viwango_
Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba ameweka jiwe la msingi la uzinduzi wa shule ya Sekondari ya Mbatakero iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro ambayo imejengwa kupitia mradi wa SEQUIP
Ujenzi wa Shule hiyo ambao umegharimu shilingi milioni 584 itasaidia kuondoa adha wanayopata wanafunzi wa eneo hilo ya kutembea umbali mrefu wa kwenda shule za jirani za sekondari za Roo na Longoi ambazo ziko umbali wa kilometa 9 kwa kila shule kutoka Kijiji cha Mbatakero na Pia itasaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi katika shule hizo.
Akizungumza baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa shule hiyo, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu amesema kuwa ujenzi wa shule hiyo ni matokeo ya maamuzi ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha anaondoa changamoto kwa wananchi
“Kama mlivyosikia, Rais Dkt. Samia anapoelezewa kuna shida, anasema viongozi watatue changamoto hiyo, ndicho kilichotokea katika shule hii ambayo wanafunzi walilazimika kutembea umbali mrefu, katika kipindi cha miaka minne amejenga zaidi ya shule 1,300 za Sekondari na amemaliza kabisa suala lililokuwa linaitwa chaguo la pili (Second Selection)”.
Katika Hatua nyingine, Dkt. Mwigulu amempongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, Dionis Myinga, Mwenyekiti wa Halmashauri Edmund Rutaraka, Mhandisi wa Halmashauri pamoja na Afisa elimu Sekondari kwa usimamizi wa Ujenzi wa Shule ya Sekondari Mbatakero na kubakiza kiasi cha shilingi Milioni 4 ambayo imetumika kununua samani za ofisi za Shule hiyo.






