Tuzo ya Kiswahili ya Safal ya Fasihi ya Afrika imetangaza orodha fupi ya miswada saba katika vipengele vitatu — riwaya, ushairi, na makusanyo ya hadithi fupi — ikiwa ni utangulizi wa hafla ya utoaji tuzo hizo kwa msimu wa 10, inayotarajiwa kufanyika Julai 24, mwaka huu, jijini Dar es Salaam.
Tuzo hiyo inadhaminiwa na kampuni ya Safal Group, kupitia kampuni zake tanzu za Mabati Rolling Mills ya Kenya na ALAF iliyoko nchini Tanzania.
Tuzo ya Kiswahili ya Safal ya Fasihi ya Afrika ilianzishwa mwaka 2014 na Dkt. Lizzy Attree na Dkt. Mukoma wa Ngũgĩ ili kutambua kazi za uandishi katika lugha za Kiafrika sambamba na kuhamasisha kazi za utafsiri kwa lugha adhimu za asili ya Kiafrika.
Tuzo hiyo, ambayo kwa mwaka huu inaadhimisha miaka 10 tangu kuanzishwa kwake mwaka 2015, imekuwa ikitolewa kila mwaka isipokuwa mwaka wa 2020, kutokana na kuweko janga la Covid 19 duniani kote.
Akizungumza wakati wa kutangaza orodha fupi ya waandishi waliofanikiwa kutinga fainali, Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa ALAF Limited, Bi Hawa Bayumi alisema “Tunapotangaza orodha hii fupi, tunayo furaha kuadhimisha miaka 10 ya tuzo hii . Hii ni hatua kubwa sana iliyopigwa na Safal Group kupitia kampuni zake tanzu yaani ALAF Limited ya Tanzania na Mabati Rollings Mills ya Kenya.
“Tunawashukuru wadau wetu wote ambao mmekuwa na sisi katika safari hii. Ni matumaini yetu kuwa mtaendelea kushirikiana na sisi huku Kiswahili kikiendelea kukua duniani,” aliongeza.
Washindi watapata zawadi kama ifuatavyo:
- Riwaya Mshindi wa kwanza 5,000 USD
- Riwaya Mshindi wa pili 2500 USD
- Ushairi mshindi wa kwanza 5000 USD
- Ushairi mshindi wa pili 2500 USD
- Mshindi hadithi fupi 2500 USD
Alieleza kuwa washindi watapata fursa ya kazi zao kuchapishwa na kampuni ya Mkuki na Nyota Publishers.
“Tayari tumeshatoa zaidi ya dola 150,000 kwa waandishi zaidi ya 40 mchango ambao umewawezesha kuchapisha zaidi ya vitabu 20 hii ikiwa ni hatua kubwa katika kutangaza lugha ya Kiswahili duniani,” alisema Bi Bayumi.
Akitangaza uamuzi wa Majaji kuhusiana na tuzo hizo, Mwenyekiti wa jopo la majaji wa tuzo kwa mwaka huu, Profesa Rayya Timammy kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi, alisema kuwa ushindani wa Tuzo ya Kiswahili ya Safal ya 2025 ya Fasihi ya Afrika ulikuwa mkubwa sana.
Profesa Timammy aliongeza, “Hali hiyo imesababishwa na idadi kubwa ya mawasilisho yaliyopokelewa kuwa na vipaji vya hali ya juu na kipekee vilivyoonyeshwa na waandishi waliowasilisha kazi zao hizo.”
Majaji wengine walioungana na Prof. Rayya Timammy katika kusoma na kuteua machapisho ambayo yatashiriki shindano la tuzo kwa mwaka wa 2025 walikuwa ni pamoja na Dkt. Masoud Mohammed wa Chuo Kikuu cha Zanzibar na aliyewahi kuwa mfanyakazi wa chuo kikuu cha Makerere Prof. Austin Bukenya.
Miswada iliyochaguliwa katika orodha fupi pamoja na waandishi ni Pamoja na:
Riwaya:
Ziaka Imetoboka – Mathew Theuri Maina (Kenya)
Mwanamkasi Ndio Basi – Salim Hussein Ng’anzi (Tanzania)
Shamba la Mawe – Dickson Damas Mtalaze (Tanzania)
Ushairi:
Diwani ya Vizikwa Vya Kale – Ali Hilal Ali (Tanzania)
Zigo la Kichwa – Maimuna Hashim Maalim (Tanzania)
Rima la Miiko na Balaa – Lenard Barnaba Mtesigwa (Tanzania)
Mikusanyiko ya Hadithi Fupi:
Mbunge Mtarajiwa na Hadithi Nyingine – Dominic Maina Oigo (Kenya)
Koti la Karani na Hadithi Nyingine – Stallone Joyfully (Tanzania)
Siri ya Mama na Hadithi Nyingine – Sophia Said Puta (Tanzania)
Washindi wa jumla watatangazwa katika sherehe ya tuzo iliyopangwa kufanyika tarehe 24 Julai, 2026, katika ukumbi wa maktaba mpya ya Chuo Kikuu Dar es Salaam.
Vigezo vya Tuzo ya Kiswahili:
Tuzo hiyo itatolewa kwa kazi ambazo hazijachapishwa au kitabu bora ambacho kilichochapishwa ndani ya miaka miwili ya mwaka wa tuzo husika katika kipengele cha hadithi za kubuni (riwaya na makusanyo ya hadithi fupi), ushairi, kumbukumbu na riwaya za michoro.
Jumla ya tuzo zilizopendekezwa za dola 15,000 za Marekani zitagawanywa kama ifuatavyo:
Mbali na zawadi hizo, machapisho yaliyoshinda pia yatapata fursa ya kuchapishwa kwa Kiswahili na kampuni ya uchapishaji ya Mkuki na Nyota iliyoko nchini Tanzania, ambapo mashairi yaliyoshinda yatatafsiriwa kwa lugha ya Kiingereza na kuchapishwa na Mfuko wa Vitabu vya Ushairi wa Kiafrika (APBF).
Kwa mwaka huu, jumla ya kazi 230 kutoka mataifa saba ziliwasilishwa kwa ajili ya kuwania tuzo hizo.
MWISHO
8888888888888888
Zaidi ya wadau 800 wathibitisha kushiriki Nanenane
Na Mwandishi weyu,Dodoma
ZAIDI ya wadau 800 wa sekta za kilimo, mifugo na uvuvi pamoja na wajasiriamali 180 wamethibitisha kushiriki katika Maonesho ya Kitaifa na Kimataifa ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi (Nanenane) 2026 yatakayofanyika katika Uwanja wa Nanenane, Nzuguni, jijini Dodoma kuanzia Agosti 1 hadi 8 mwaka huu.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, ameyasema hayo jana, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya maonesho hayo, akieleza kuwa Mkoa wa Dodoma kwa kushirikiana na Mkoa wa Singida, unaounda Kanda ya Kati, umepewa heshima ya kuandaa maonesho hayo kwa mara ya tatu mfululizo.
Alisema maonesho ya Nanenane ni jukwaa muhimu la kuonesha teknolojia, ubunifu na fursa za uwekezaji katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi, pamoja na kuongeza tija, thamani ya mazao na ushindani katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Kwa mujibu wa Senyamule, washiriki waliothibitisha kushiriki ni pamoja na halmashauri za Mikoa ya Dodoma na Singida, wizara mbalimbali, mashirika ya umma, kampuni za mitambo na zana za kilimo, kampuni za pembejeo, viwanda vya kusindika mazao, kampuni za nishati na mawasiliano, taasisi za fedha, mashirika yasiyo ya kiserikali .
Vile vile alisema pia watakuwepo wadau wa kimataifa kutoka nchi za China, India, Israel, Japan, Urusi, Belarus, Uholanzi, Sweden, Switzerland, Saudi Arabia, Uingereza, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Kenya.
Aidha, alisema wajasiriamali 180 tayari wamejisajili kushiriki kwa kuonesha bidhaa na huduma mbalimbali kwa lengo la kupanua masoko, kukuza biashara zao na kuongeza kipato.
Katika kuhamasisha ushiriki wa vijana, amesema Wizara ya Kilimo itagharamia banda maalumu litakalowawezesha vijana kuonesha bunifu zao katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi, huku akiwahimiza kujisajili kupitia mfumo uliowekwa ili kunufaika na fursa hiyo.
Xxx



