*Ni katika muendeleo wa vikao kazi kati ya TANESCO na Madiwani Wilaya ya Kahama
*Awataka Madiwani kuwa mstari wa mbele kuwaelimisha wananchi wa maeneo yao
Katika kuhakikisha ajenda ya nishati safi ya kupikia inatekelezwa kwa vitendo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kahama Bi. Glory Absalum, amewataka madiwani kuwa mabalozi wa mabadiliko kwa kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kutumia nishati ya umeme kupikia ambayo ni salama kiafya, nafuu na inalinda mazingira.
Akizungumza Februari 17, 2026 kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Kahama wakati wa ufunguzi wa kikao kazi kati ya TANESCO na madiwani wa kata 20 za Wilaya hiyo, Bi. Glory amesisitiza kuwa upatikanaji wa umeme ni fursa muhimu katika kuboresha maisha ya wananchi.
“Tunamshukuru sana Mhe. Rais kwa kuendelea kutuletea miradi ya umeme inayorahisisha upatikanaji wa nishati. Leo hii kina mama wanaweza kupika kwa umeme wakiwa salama, wakitunza afya zao na mazingira. Matumizi ya umeme yanapunguza utegemezi wa kuni na mkaa na hivyo kulinda misitu yetu,” alieleza Bi. Glory.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Kahama Mjini, Mhe. Benjamin Ngayiwa, amewataka madiwani kushirikiana kwa karibu na TANESCO kulinda miundombinu ya umeme ambapo amebainisha kuwa uharibifu wa miundombinu unaofanywa na watu wasio waaminifu ni moja ya sababu zinazoathiri upatikanaji wa huduma bora ya umeme.
Naye Meneja wa TANESCO Shinyanga , Mha. Khadija Mbaruku, amewashukuru viongozi hao kwa kuitikia wito wa kikao kazi hicho na kuahidi ushirikiano ili kuhakikisha umeme unawafikia wananchi kwa wakati na kwa kuzingatia vipaumbele vya maendeleo.
“Tunawashukuru kwa kutenga muda wenu kushiriki kikao hiki. TANESCO itaendelea kushirikiana nanyi kuhakikisha huduma ya umeme inaboreshwa, huku tukitoa kipaumbele katika taasisi za kijamii kama shule, zahanati na nyumba za ibada,” alisisitiza Mha. Khadija.
Kikao kazi hicho kimehudhuriwa pia na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kahama, Mhe. Mataluma Kaniki, kikilenga kuwajengea uwezo madiwani kuhusu shughuli na mipango ya TANESCO katika maeneo yao.
.







