Waziri wa ulinzi wa Japani amesema anapanga kupeleka makombora kwenye kisiwa chake cha magharibi karibu na Taiwan ifikapo Machi 2031, huku mvutano wa kikanda ukiendelea.

Ni mara ya kwanza kwa Japani kubainisha ratiba ya kupelekwa kwa kombora katika kisiwa cha Yonaguni.

Yonaguni iko umbali wa kilomita 110 tu (maili 68) kutoka Taiwan.

Mvutano kati ya Tokyo na Beijing umekuwa mkubwa tangu Novemba wakati Waziri Mkuu wa Japani Sanae Takaichi alipopendekeza kwamba Japani itakuwa tayari kujilinda iwapo kutakuwa na shambulio dhidi ya Taiwan.

Wasiwasi ni kwamba shambulio lolote dhidi ya Taiwan, ambayo ni mshirika wa Marekani, linaweza kusababisha mzozo wa moja kwa moja wa kijeshi kati ya Washington na Beijing, kisha likaenea hadi kujumuisha washirika wengine wa Marekani katika eneo hilo kama vile Japani.

Waziri wa ulinzi wa Japan Shinjiro Koizumi alitangaza ratiba ya makombora hayo siku ya Jumanne, siku moja baada ya China kuweka vikwazo vya usafirishaji nje kwa makampuni na mashirika 20 ya Japani.

Koizumi alisema kitengo cha Yonaguni kitakuwa na makombora ya masafa ya kati yanayoweza kuzuia ndege na makombora.

Matukio ya hivi punde yanakuja baada ya Takaichi, mhafidhina, kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa bunge mapema mwezi huu.

Ushindi huo ulimpa Takaichi nafasi ya kisiasa ya kuongeza nguvu katika kuimarisha uwezo wa ulinzi wa Japani.