WAZIRI wa Mambo ya Nje wa Marekani asema Iran inaendeleza makombora ya masafa marefu yanayoweza kufikia Marekani, akisisitiza kuwa hilo ni tishio lisilovumilika kabla ya mazungumzo ya Geneva.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, amesema Iran inaendelea kutengeneza makombora ya masafa marefu yanayoweza siku moja kufikia Marekani, akielezea mpango huo kama “tishio lisilovumilika.” Alizungumza na waandishi wa habari mjini Basseterre, St Kitts na Nevis.

Alishangazwa na uamuzi wa Tehran kuendelea kuwekeza katika makombora ya masafa marefu licha ya vikwazo vya kiuchumi na changamoto kubwa za kifedha.

Kauli hiyo imekuja kabla ya duru nyingine ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Marekani na Iran mjini Geneva. Mazungumzo hayo, yanayopatanishwa na Oman, yanatarajiwa kujikita zaidi katika mpango wa nyuklia wa Iran unaobishaniwa.

Rubio alisema diplomasia bado ni chaguo, akisisitiza kuwa Rais Donald Trump anapendelea suluhisho la mazungumzo. Hata hivyo, alionya kuwa kukataa kwa Iran kujadili mpango wake wa makombora ya balistiki kunasalia kuwa “tatizo kubwa” katika kufikia makubaliano.