Israel imesema imeanzisha wimbi jingine la mashambulizi dhidi ya Iran, leo Jumapili huku hali ya sintofahamu ikiendelea miongoni mwa Wairani baada ya kifo cha Kiongozi Mkuu wa nchi hiyo, Ayatollah Ali Khamenei.

Vyombo vya habari vya serikali ya Iran vilithibitisha kuwa Khamenei, mwenye umri wa miaka 86, amefariki pamoja na Mkuu wa Majeshi ya Iran, Abdolrahim Mousavi katika mashambulizi ya pamoja ya Marekani na Israel. Rais wa Marekani, Donald Trump, ameonya kuwa iwapo Iran italipiza kisasi, itakabiliwa na nguvu ambayo haijawahi kushuhudiwa.

Iran imetangaza kuunda baraza la uongozi la muda, huku maafisa wake wakilaumu Marekani na Israel kwa kutaka kuidhoofisha nchi hiyo. Bunge la Iran limeonya kuwa Marekani na Israel “watalipa gharama” kwa kuvuka mstari mwekundu.

Aidha Iran imerusha makombora kulenga vituo vya Marekani nchini Iraq na katika mataifa ya Ghuba, na milipuko mikubwa imeripotiwa kusikika Dubai na Doha. Katika Israel, ving’ora vya mashambulizi ya anga vimesikika mara kadhaa, huku mfumo wa ulinzi wa anga ukijaribu kuzuia makombora ya Iran. Lakini hakuna taarifa za majeruhi.

Mvutano huo unaendelea kuongezeka, huku pande zote zikiahidi kuendeleza mashambulizi, jambo linalozua hofu ya vita pana katika kanda hiyo muhimu kwa uzalishaji wa mafuta duniani.