Israel imesema imeanzisha wimbi jipya la mashambulizi katikati mwa Tehran, ikilenga kufikia kitovu cha mji mkuu na kutawala anga ya Iran, baada ya wimbi la kwanza lililomuua Kiongozi Mkuu wa taifa hilo.
Milipuko mikubwa imeripotiwa Jumapili mjini Tehran huku mashambulizi ya Marekani na Israel yakiingia siku ya pili mfululizo. Jeshi la Israel limesema limefanikiwa kuvunja sehemu kubwa ya mifumo ya ulinzi wa anga magharibi na kati mwa Iran, hatua inayodaiwa kufungua “njia kuelekea Tehran.”
Msemaji wa jeshi la Israel, Luteni Kanali Nadav Shoshani, amesema bado kuna malengo mengi yakiwemo viwanda vya uzalishaji wa silaha na miundombinu ya kijeshi. Amesema Israel ina uwezo wa kuendelea na operesheni kwa muda wowote utakaohitajika, lakini kwa sasa hakuna mpango wa kupeleka vikosi vya ardhini nchini Iran. Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz, ametaja kuuawa kwa Khamenei kuwa hatua muhimu ya kimkakati.
“Yeye ndiye aliyeongoza kampeni ya uharibifu dhidi ya Taifa la Israel, aliunda mhimili mzima wa uovu unaotuzunguka, na hata ndani ya Iran aliongoza msimamo mkali usio na maridhiano dhidi ya Taifa la Israel. Kwa hiyo, kuondolewa kwake ni hatua ya mabadiliko makubwa, pamoja na maafisa wengine wengi waandamizi na muhimu walioondolewa pamoja naye.”
Vyombo vya habari vya Iran vimethibitisha kuwa Ayatollah Ali Khamenei, aliyekuwa madarakani tangu 1989, aliuawa akiwa ofisini kwake katika mashambulizi ya Jumamosi. Shambulio hilo pia liliwaua maafisa wa juu akiwemo Mkuu wa Majeshi Abdolrahim Mousavi. Aidha, shirika la habari la ILNA limeripoti kuwa rais wa zamani wa Iran, Mahmoud Ahmadinejad, ameuwawa katika shambulio la anga mjini Tehran pamoja na mlinzi wake.



