Na. Benny Mwaipaja, Dar es Salaam

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) Serikali inatambua na kusisitiza umuhimu wa kuimarisha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (Public Private Partnership – PPP) kama njia muhimu ya kuongeza rasilimali Fedha na kuharakisha utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo nchini.

Mhe. Balozi Omar alisema hayo wakati akifungua rasmi Kozi Fupi ya Kumi na Saba ya Viongozi (Capstone 17) yanayotolewa na Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC) kilichoko Kunduchi, jijini Dar es Salaam.

Mhe. Balozi Omar, amesema kuwa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi ni fursa muhimu ambayo bado haijatumika kikamilifu katika kuendeleza miradi ya umma.

“Serikali imekuwa ikitumia njia mbalimbali za kupata fedha za maendeleo ikiwemo ukusanyaji wa kodi na maduhuli, uwekezaji wa sekta binafsi pamoja na mikopo ya ndani na nje ya nchi, hata hivyo vyanzo hivi vina mipaka kutokana na hali ya uchumi na masharti ya kudhibiti kiwango cha deni la taifa” alisema Mhe. Balozi Omar.

Aliongeza kuwa kwa muda mrefu Sera ya Bajeti imeweka lengo la kuhakikisha nakisi ya bajeti haizidi asilimia tatu ya Pato la Taifa, jambo linaloweka ukomo wa matumizi ya mikopo kugharamia miradi ya maendeleo, hivyo PPP inaweza kuwa suluhisho muhimu la kusaidia Serikali kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati bila kuongeza mzigo mkubwa wa kifedha kwa taifa.

Aidha alisema Serikali imepanga kutekeleza miradi mikubwa ikiwemo reli mpya ya kisasa ya SGR kutoka Tanga hadi Musoma kupitia Arusha pamoja na reli ya Mtwara hadi Ludewa kupitia Mbamba Bay, sambamba na kuongeza maradufu uwezo wa uzalishaji wa nishati ifikapo mwaka 2030 na miradi hiyo inahitaji rasilimali kubwa za kifedha hivyo kutoa nafasi pana kwa ushiriki wa sekta binafsi kupitia PPP.

Mhe. Balozi Omar aliwataka washiriki wa kozi hiyo kutumia mafunzo wanayopata kuchambua kwa kina fursa zilizopo katika miradi ya PPP, ikiwemo aina mbalimbali za ubia huo, faida zake na vihatarishi vinavyoweza kujitokeza, hasa katika maeneo yanayohusiana na usalama wa taifa.

“Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeweka kipaumbele kikubwa katika kuimarisha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi kama njia ya kuchochea ukuaji wa uchumi na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi” alisema Mhe. Balozi Omar.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC), Meja Jenerali Wilbert Ibuge, alisema kuwa Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC) kimeendelea kusisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi katika kuchochea maendeleo endelevu ya Taifa kupitia Kozi Fupi ya 17 (Capstone 17) inayofanyika kwa siku tano.

Alisema kuwa mafunzo hayo yanalenga kujenga uelewa wa pamoja kwa viongozi na watendaji waandamizi kutoka sekta mbalimbali kuhusu masuala ya kimkakati yanayohusu usalama na maendeleo ya Taifa.

Kaulimbiu ya Kozi ya 17 ni “Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi Tanzania katika Kuchochea Maendeleo Endelevu ya Taifa”, ikilenga kuangazia nafasi ya ushirikiano huo katika kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Kwa mujibu wa maelezo hayo, Dira ya Maendeleo 2050 inalenga kuifanya Tanzania kuwa nchi ya kipato cha kati cha juu ifikapo mwaka 2050, ikiwa na uchumi shindani unaotegemea viwanda, rasilimali zake na nguvukazi yenye ujuzi na ubunifu.

Kozi hiyo ya siku tano inahusisha mihadhara, mijadala ya vikundi, uchambuzi wa changamoto na fursa za ubia wa sekta ya umma na binafsi (PPP), pamoja na ziara za kujifunza katika miradi ya kimkakati.

Jumla ya washiriki 82 kutoka wizara mbalimbali, taasisi za umma na binafsi pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama wanashiriki katika kozi hiyo, inayolenga kuimarisha uelewa na ushirikiano katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya Taifa.

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (kushoto), akikabidhiwa tuzo maalumu na Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC), Meja Jenerali Wilbert Ibuge, kama Ishara ya kutambua mchango wake katika chuo hicho wakati alipowasili kwa ajili ya kufungua Kozi Fupi ya Kumi na Saba ya Viongozi (Capstone 17) ya Chuo hicho, inayohusu Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (Public Private Partnership – PPP), katika kuchochea Maendeleo Endelevu, hafla iliofanyika katika Chuo hicho Kunduchi, jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (Katikati aliyeketi), Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC), Meja Jenerali Wilbert Ibuge (wa tatu kushoto), Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba (wa pili kulia aliyeketi) Kansela wa Chuo hicho, Dkt. Abdulhamid Yahya Mzee (wa tatu kulia aliyeketi), wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali wa umma wanaoshiriki Kozi Fupi ya Kumi na Saba ya Viongozi (Capstone 17) ya Chuo hicho, inayohusu Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (Public Private Partnership – PPP), katika kuchochea Maendeleo Endelevu, hafla iliofanyika katika Chuo hicho Kunduchi, jijini Dar es Salaam. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Dar es Salaam)