WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema kuwa Serikali inatambua uwepo wa watumishi wa umma wanaochapakazi na kuwataka kuendelea kufanya kazi kwa bidii na uadilifu huku wakijiepusha kujiingiza katika makundi ya wazembe, wezi na wanaofanya kazi kwa mazoea.
“Serikali haitomuonea mtu, watumishi wachapakazi wasiingie ubaridi kwa sababu Serikali inatambua mchango wao katika maendeleo ya Taifa. Watu wasome alama za nyakati Serikali haitovumilia masuala ya wizi kwa sababu yanarudisha nyuma maendeleo.”
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo Jumatatu, Machi 09, 2026 wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kata ya Namanyere wilayani Nkasi akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Rukwa. Miongoni mwa malengo ya ziara hiyo ni kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Dkt. Mwigulu ametumia fursa hiyo kuwasisitiza watumishi wa umma kufanya kazi kwa weledi na kujiepusha na vitendo vya udokozi kwa sababu havikubaliki na havivumiliki, hivyo wahakikishe wanatekeleza majukumu yao ikiwemo kusimamia ipasavyo ujenzi wa miradi.
Pia, Waziri Mkuu amesisitiza mikoa yote kuhakikisha katika upangaji wa bajeti wanaweka vipaumbele vya uchimbaji wa visima kupitia mitambo iliyosambazwa katika mikoa yao. “Mitambo ya uchimbaji maji itumike kuchimba visima ili wananchi wapate maji ya uhakika.”
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amezitaka mamlaka husika kuangalia uwezekano wa kuweka utaratibu au sheria itakayowabana wakandarasi kuhakikisha wanawalipa wafanyakazi wao stahiki zao kwa wakati.
Ametoa agizo hilo kutokana na kumekuwapo kwa malalamiko ya baadhi ya wakandarasi kutowalipa wafanyakazi wanaofanya kazi katika miradi ya ujenzi hata pale wanapokuwa wameshalipwa na Serikali kwa kazi walizotekeleza.
Mheshimiwa Dkt. Mwigulu ametoa agizo hilo baada ya wananchi waliofanykazi katika miradi mbalimbali kueleza kero ya kutolipwa na wakandarasi licha ya wakandarasi hao kuwa tayari wamelipwa na Serikali.
Kwa upande wao, wabunge wa mkoa wa Rukwa wameipongeza Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa utekelezwaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika maeneo yao ikiwemo ya afya, elimu na kilimo.
Miongoni mwa wabunge hao ni Mbunge wa Nkasi Kaskazini Salum Kazukamwe ambaye alishukuru kwa ujenzi wa hospital ya wilaya ambayo inakwenda kurahisisha upatikanaji wa huduma bora za afya, ambapo pia, mbunge huyonameiomba Serikali kumalizia ujenzi wa kituo cha afya cha Kebwe.




