Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Mbeya
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), James Kaji, ameongeza mashine na siku za usajili wa Vitambulisho vya Taifa katika Mkoa wa Mbeya kufuatia mwitikio mkubwa wa wananchi wanaojitokeza kujiandikisha kupata Namba ya Utambulisho wa Taifa (NIN).
Wakati wa ziara yake ya kukagua zoezi la usajili mkoani humo, amesema ameridhishwa na mwamko mkubwa wa wananchi wanaojitokeza kujiandikisha, hali inayoonesha uelewa unaoongezeka kuhusu umuhimu wa utambulisho wa Taifa katika kupata huduma mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
Kwa mujibu wa takwimu za zoezi hilo, zaidi ya wananchi 7,400 tayari wamehudumiwa ndani ya siku chache zilizopita, huku wastani wa zaidi ya wananchi 400 wakisajiliwa kila siku katika zoezi maalum la usajili.
Akizungumza wakati wa ziara yake, kiongozi huyo aliwaomba wananchi kuhakikisha wanachukua vitambulisho vyao vya Taifa vilivyokwisha chapishwa ili kuepuka kusitishwa kwa matumizi ya namba zao za utambulisho.
Kwa mujibu wa takwimu za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), katika Mkoa wa Mbeya pekee zaidi ya vitambulisho 130,000 bado havijachukuliwa na wamiliki wake.
Aidha, kutokana na mwitikio huo mkubwa, Mkurugenzi Mkuu ameongeza siku 10 zaidi za usajili ili kuwapa wananchi wengi fursa ya kujiandikisha na kupata Namba ya Utambulisho wa Taifa.
Ameagiza pia kuongezwa kwa watendaji katika vituo vya usajili pamoja na kuwekwa kwa viti na mahema katika maeneo ya huduma ili kupunguza adha kwa wananchi wanaosubiri kupatiwa huduma.




