Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ameielekeza Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) ,mkoani Pwani kuweka utaratibu mzuri wa mgawanyo wa rasilimali fedha katika halmashauri na wilaya kwa kuzingatia uhalisia na vipaumbele ili kuondoa hisia hasi kwa viongozi na wananchi.
Ulega alitoa maelekezo hayo alipozungumza na wadau wa sekta ya barabara, viongozi mbalimbali Halmashauri na Wilaya, wabunge pamoja na watendaji wa TARURA na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoani humo.
Alieleza ingawa TARURA haipo moja kwa moja chini ya Wizara ya Ujenzi, yeye ni msimamizi wa barabara zote nchini kwa mujibu wa sera, sheria, huku akieleza kuwa usimamizi wa wakala huo umekasimiwa TAMISEMI.

“TANROADS ina fomula nzuri ya mgawanyo wa fedha za utekelezaji wa miradi ya barabara lakini nielekeze TARURA na TANROADS kuweka utaratibu mzuri wa kugawa keki iliyopo ” alieleza Ulega.
Aidha alieleza kipaumbele kikubwa ni kuunganisha na kuufungua Mkoa wa Pwani kupitia barabara za Tamco–Mapinga–Bagamoyo, Bagamoyo–Makofia–Mlandizi–Mzenga na Kibaha–Kisarawe, pamoja na kurahisisha usafiri kwa wananchi wanaotoka Mkuranga, Kibiti na Rufiji kwenda makao makuu ya mkoa bila kulazimika kupita Dar es Salaam.
Ulega alieleza , barabara hizo zitapatiwa fedha katika bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027 ili kuanza ujenzi.
Kadhalika, alisema serikali itatoa kipaumbele kwa miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo barabara ya Mailmoja Kibaha yenye urefu wa kilomita 3.6, akisema itasaidia kuboresha sura ya makao makuu ya Mkoa na barabara ya Kitaifa.

Kuhusu ombi la Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo CPA Subira Mgalu la kuboresha barabara ya Afrika Mashariki Pangani–Makurunge kipande cha Mkange kuunganisha na barabara ya Tanga–Pangani, Ulega alisema mradi huo umefikia asilimia 60 ya utekelezaji, mkandarasi akifikia asilimia 80, serikali itaweza kuomba fedha za ziada kwa ajili ya kukamilisha utekelezaji wa ombi hilo.
Awali, Mgalu aliishukuru Serikali kwa kuimarisha mtandao wa barabara na kuiomba itathmini miradi yenye wakandarasi na ile iliyoachwa viporo ili ikamilishwe na kurejesha matumaini kwa wananchi.
Vilevile Mgalu pamoja na Diwani wa Kata ya Yombo Muhammed Usinga waliomba, barabara ya Kongowe–Yombo ipandishwe hadhi na kujengwa kwa kiwango cha lami ili kurahisisha usafiri kwenda Bagamoyo sambamba na mradi wa taa za barabarani Bagamoyo.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete alisema kwa miaka mitatu mfululizo jimbo hilo halijapata utekelezaji wa miradi ya barabara kupitia TARURA wala fedha za miradi hiyo, hivyo kuomba utekelezaji mzuri utakaosaidia wananchi waweze kunufaika na mgawanyo wa fedha.

Mbunge wa Jimbo la Kisarawe Dkt. Suleiman Jafo aliwataka wataalamu, kufanya tathmini ili kuhakikisha kila halmashauri na wilaya inanufaika na fedha za miradi ya barabara.
“Yapo maeneo ya vipaumbele yazingatiwe, kuna wananchi wanakwama; kule Kisarawe ilibidi nichukue greda kuchonga kilomita 120 kwa fedha zangu, hivyo taasisi husika ziangalie namna bora ya kugawa hii keki ili kuleta manufaa kwa jamii,” alieleza Jafo.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge alisema mkoa huo una viwanda 1,688, huku katika kipindi cha uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan vikijengwa viwanda vipya 301, ambapo kati ya hivyo 235 ni vikubwa na vya kati.
Alielezea, ukuaji huo wa uwekezaji unaifanya miundombinu ya barabara kuwa muhimu zaidi ili kuendana na kasi ya maendeleo ya uchumi wa mkoa.

“Naamini Meneja wa TARURA Mkoa wa Pwani Ibrahim Kibassa na Meneja wa TANROADS Mkoa wa Pwani Mhandisi Baraka Mwambage wataendeleza kazi nzuri iliyofanyika ili kuendana na kasi ya maendeleo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,” alielezea Kunenge.
Akizungumzia ombi la kupandisha hadhi barabara ya Kongowe–Yombo–Bagamoyo, Meneja wa TARURA Mkoa wa Pwani Ibrahim Kibassa alisema tayari ujenzi wa kiwango cha lami umeanza ambapo umefikia mita 760 sawa na asilimia 90.
Kuhusu barabara ya Kongowe–Soga yenye urefu wa kilomita 17.5 inayoelekea katika kituo cha reli ya mwendokasi (SGR) na kiwanda cha nyama cha Tanchoice, Kibassa alifafanua TARURA imeandaa mkakati wa kufanya usanifu kwa kiwango cha lami huku ikiendelea na maboresho ya muda kwa kuweka changarawe.
Anaeleza hadi sasa TARURA Pwani imeongeza mtandao wa barabara za lami kutoka km 84.14 hadi 122.41, barabara za changarawe kutoka km 588.773 hadi 871.392, makaravati kutoka 2,294 hadi 3,590 na uwekaji wa taa za barabarani 1,099.





