Na Stella Aron, JamhuriMedia, Njombe

Wakala wa Umeme Vijijini (REA),imefadhili miradi mitano ya uzalishaji umeme katika Mkoa wa Njombe na kuchangia kupunguza kero ya ukosefu wa umeme pamoja na kuchochea maendeleo ya wananchi.

Hayo yamebainishwa leo Machi 10, 2026 na Kaimu Meneja Usaidizi wa Kiufundi wa REA, Mhandisi Emanuel Yesaya, wakati wa ziara iliyoshirikisha wahariri waliotembelea Kituo cha kuzalisha umeme cha Ijangala kilichopo Kijiji cha Masisiwe, Kata ya Ukwama wilayani Makete mkoani Njombe unaoendeshwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kusini Kati kupitia kituo cha Diakonia cha Tandala.

Miradi hiyo inayozalisha jumla ya megawati tatu, ambazo huingizwa kwenye Gridi ya Taifa imesaidia kuchochea shughuli za kiuchumi katika mkoa huo.

Mhandisi Yesaya amesema miradi hiyo inasaidia kuongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika pamoja na kutoa ajira kwa wananchi.

“REA imekuwa ikifanya jitihada za kuhakikisha kuwa umeme unafika kila Kijiji. Mradi huu wa Ijangala unanufaisha wananchi katika vijiji saba kwa kupata umeme wa uhakika, mkakati wa REA ni kuhakikisha umeme unawafikia wananchi wa vijiji vyote na tayari huduma hiyo imefanikiwa.

“Bado kuna vitongoji havijafikiwa na huduma ya umeme nchini lakini kuna jitihada kubwa zinazofanyika ili vitongoji viivyobaki vinufaike na huduma hiyo,” amesema mhandisi Yesaya.

Ameongeza kuwa Mradi wa Umeme wa Ijangala ( Ijangala Mini Hydropower Plat 360 kW) wakati wa ujenzi wake REA ilitoa ruzuku ya Sh.bilioni 1.6 ambazo zimesaidia ujenzi wa miundombinu.

“Serikali kupitia REA imesaidia kuongeza uwekezaji katika miradi ya umeme vijijini nia ni kuongeza uzalishaji wa umeme katika Gridi ya Taifa. Mradi huu umepata mkopo kutoka REA wenye masharti nafuu wa Sh milioni 922,” amesema Yesaya.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Kiongozi wa Dayosisi hiyo, Mchungaji Silvia Sanga amesema wazo la kuanzisha mradi huo lilitokana na changamoto ya ukosefu wa umeme wa uhakika katika eneo hilo.

Amesema awali walikuwa wakitumia gharama kubwa za uendeshaji kwa kutumia jenereta la umeme ambapo walikuwa wakitumia gharama kubwa za mafuta lakini kwa sasa gharama za uendeshaji zimekuwa ndogo tangu kuanza uzalishaji umeme Machi mwaka jana.

“Hili wazo la kuanzisha kituo hii lilitoka kwa viongozi wa KKKT hapa kijijini kwenye kijiji chetu cha Masisiwe na kisha tukaishirikisha Serikali, tunashukuru tangu kuanza kwa mchakato wake mpaka kukamilika chini ya ufadhili wa REA umekuwa na manufaa makubwa” amesema mchungaji Silvia.

Naye Meneja wa mradi huo, Daudi Sanga, amesema mradi huo unasaidia wananchi katika vijiji saba vya eneo hilo ambapo kwa mwezi mradi huo unazalisha zaidi ya uniti 120,000 na matarajio ni kufikia zaidi ya uniti 200,000 kwa mwezi.

Tulibhosa Andrew ni mkazi wa Kijiji cha Masisiwe, ameishukuru Serikali kwa ufadhili wa mradi huo kwani tangu upatikanaji wa umeme wa uhakika umekuwa na manufaa makubwa kwake.

“Tunaipongeza Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwani tulikuwa gizani lakini kwa sasa tunafanya shughuli zetu hadi usiku na bila wasiwasi” amesema.

Naye Christian Joseph, amesema kuwa awali shughuli zilikuwa ni za kusuasua hasa kipindi cha mvua kutokana na kuwepokwa giza na kuchangia kufunga biashara mapema.

“Mvua zinaponyesha huwa kuna giza,unaweza zikapita siku tatu jua lisionekane, na kuna baridi sana, lakini kwa sasa tuna uwezo wa kuchemsha chai kwa muda mchache” amesema.