Na Mwandishi Wetu, JamhutiMedia, Karatu
Serikali kupitia Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imetekeleza mradi wa ujenzi wa daraja la mawe la Sabasaba lenye urefu wa mita 16.6 na upana wa mita 7 katika eneo la Kambi ya Simba, Wilaya ya Karatu kwa gharama ya Shilingi milioni 81.
Ujenzi huo ni sehemu ya utekelezaji wa mfuko wa Dharura (CERC) unaofadhiliwa na Benki ya Dunia unaolenga kurejesha na kuboresha miundombinu iliyoharibiwa na mafuriko.
Sambamba na mradi huo, Serikali inaendelea na ujenzi wa barabara ya udongo ya Manyara–Lositeteya yenye urefu wa kilomita 10, ambapo hadi sasa kilomita 3.5 utekelezaji wake unaendelea.
Akizungumza na waandishi wa habari wilayani Karatu, Meneja wa TARURA Wilaya ya Karatu, Mhandisi Msetu Madara, alisema awali barabara hiyo ilikuwa na changamoto kubwa ya kupitika kufuatia mafuriko ya mwaka 2024/2025.
Alisema ujenzi wa daraja hilo umeondoa changamoto ya usafiri na kurahisisha usafirishaji wa mazao kwa wananchi wa vijiji vya Kambi ya Simba, Slahhamo, Upper Kitete, Lositete na vitongoji vyake.
“Kwa sasa wananchi wanaweza kusafirisha mazao yao kwa urahisi ndani na nje ya eneo lao. Daraja hili limejengwa kwa kutumia mawe na pia tumejenga mitaro ya maji ili kuzuia maji yasituame katika mashamba na barabarani,” alisema Madara.
Aliongeza kuwa matumizi ya teknolojia ya ujenzi wa madaraja ya mawe yamesaidia kupunguza gharama za ujenzi kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na ujenzi wa madaraja ya zege
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Slahhamo, Ombeni Panga, aliishukuru Serikali kwa kutekeleza mradi huo na kusema mradi huo umekuwa na manufaa makubwa kwa wananchi wa eneo hilo.
Alisema hapo awali walikuwa wakitumia kalavati ambazo zilikuwa zikisombwa na maji wakati wa mvua kubwa, lakini sasa hata katika msimu huu wa mvua barabara hiyo inapitika bila matatizo.
“Maji yanayotiririka hapa yanatoka katika msitu wa Ngorongoro na huwa mengi sana. Pia udongo wa eneo hili ni wa mfinyanzi na kuna milima mingi, hivyo barabara ilikuwa mbaya na wakati mwingine haikupitika kabisa. Kwa sasa wananchi na wanafunzi wanapita bila kizuizi,” alisema.
Mkazi wa Kijiji cha Slahhamo, Edward Juma, alisema mradi huo pia umechangia kutoa ajira kwa vijana pamoja na kuwapatia ujuzi wa ujenzi wa daraja la mawe.
“Tumepata ajira na kujifunza ujuzi ambao utatusaidia kupata kazi nyingine baadaye. Mimi natokea Moshi na ninashukuru kupata nafasi ya kufanya kazi katika mradi huu,” alisema.
Naye, mkazi mwingine wa kijiji hicho, Criscent Sarawati, alisema kabla ya ujenzi wa daraja hilo mashamba yao yalikuwa yakijaa maji mengi wakati wa mvua, lakini baada ya ujenzi huo hali imeimarika.
Alisema pia gharama za usafiri kutoka eneo hilo kwenda Karatu zimepungua kutoka Sh 5,000 hadi Sh 3,000, jambo linalorahisisha usafirishaji wa mazao kwenda sokoni.
Mkazi mwingine, Bi. Febrania Thomas, alisema uboreshaji wa barabara hiyo umeleta nafuu kwa wananchi kwa kuwa sasa wanaweza kusafirisha mazao yao kwa urahisi zaidi na kwa gharama ndogo.


