Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

Takribani asilimia 79 ya nguvu kazi ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) ni vijana, hatua inayotafsiri dhamira ya Serikali ya kutoa nafasi kwenye kundi hilo kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya sekta ya nishati na uchumi wa taifa.

Hayo yameelezwa leo Machi 11,2026 na Mkurugenzi wa TPDC, Mussa Makame, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusu mchango wa miradi ya nishati katika kufungua fursa za ajira, mafunzo na ushiriki wa vijana katika miradi mikubwa ya maendeleo.

Makame amesema utekelezaji wa miradi mbalimbali ya nishati nchini unaendelea kutoa ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, sambamba na kuwajengea vijana ujuzi na uzoefu unaohitajika katika sekta hiyo muhimu ya uchumi.

“Asilimia 79 ya nguvu kazi ya TPDC ni vijana,hii inaonesha wazi dhamira ya Serikali kuwaamini na kuwapa nafasi vijana wa Kitanzania kushiriki kikamilifu katika kuendesha sekta ya nishati,” amesema Makame.

Ameeleza kuwa pamoja na ajira, vijana pia wananufaika kupitia zabuni za utoaji wa huduma mbalimbali katika miradi ya nishati ikiwemo uhandisi, usafirishaji, ujenzi, ugavi, teknolojia pamoja na huduma za kitaalamu.

Aidha, amesema TPDC inaendesha programu maalum ya mafunzo kwa vitendo (Internship) inayowapatia takribani vijana 60 kila mwaka nafasi ya kupata uzoefu katika usimamizi na uendeshaji wa sekta ya nishati, hususan katika sekta ndogo ya gesi asilia.

Kwa mujibu wa Makame, utekelezaji wa miradi hiyo pia umechochea ukuaji wa sekta nyingine za kiuchumi kama viwanda, usafirishaji na huduma za hoteli, hali inayotoa fursa kwa vijana kujiajiri au kupata ajira katika maeneo mbalimbali ya uchumi.

Akizungumzia Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), Makame amesema maandalizi yanaendelea kuwajengea uwezo vijana watakaoshiriki katika uendeshaji wa mradi huo pindi utakapoanza uzalishaji.

Amesema kupitia programu maalum ya maandalizi ya wataalamu wa mradi huo, vijana 138 tayari wamepata mafunzo ya vitendo katika taasisi mbalimbali ikiwemo VETA, Arusha Technical College pamoja na Uganda Petroleum Institute Kigumba.

Aidha, vijana hao wamepata uzoefu kupitia miradi ya viwanda vya kuchakata gesi asilia ya Madimba na Songo Songo pamoja na mradi wa bomba la kusafirisha gesi kutoka Mtwara na Lindi hadi Dar es Salaam, ikiwa ni maandalizi ya kuwashirikisha kikamilifu katika utekelezaji wa mradi wa EACOP.