Na Stella Aron, JamhuriMedia, Njombe
Ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme wa Lupali unaotumia nguvu ya maporomoko madogo ya maji ya mto Lupali umefikia asilimia 99 ambao ukikamilika utaingizwa kwenye gridi ya taifa kilowati 317 na kuchangia upatikanaji umeme wa uhakika mkoani Njombe.
Hayo yamebainishwa na Kaimu Meneja Usaidizi wa Kiufundi kwa Waendelezaji wa Mradi kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Emmanuel Yesaya wakati wa ziara ya kutembelea miradi ya REA inayotekelezwa katika mkoa huo sambamba na kupitia maendeleo ya waendelezaji wadogo wa miradi ya kuzalisha umeme hapa nchini na kupatiwa ufumbuzi iliyoshrikisha wahariri kutoka Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF).
Amesema kuwa katika kufanikiha mradi huo Wakala wa Nishati Vijijini (REA), imetoa kiasi cha shilingi bilioni 5.4 kwenye mradi wa kuzalisha umeme wa maji Lupali wenye uwezo wa kuzalisha kilowati 317 unaotekelezwa na shirika la Benedictine Sisters of St. Gertrud Convent Imiliwaha.
“Fedha zilizotolewa na REA zimewezesha tafiti za mradi, ujenzi wa kituo cha uzalishaji wa umeme na miundombinu ya usambazaji kwenye kituo cha Imiliwaha Sisters Convent ambapo utasaidia vijiji vya jirani vya Boimanda, Kitulila na Matola kupata umeme wa hakika.
“Utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 99 ambapo kazi zilizotekelezwa hadi sasa ni pamoja na ujenzi wa kizuizi cha maji na mtaro wa kupitisha maji ya mafuriko ambao tayari umekamilika na baada ya miezi mitatu uzalishaji utaanza” amesema.
Mhandisi Yesaya amezishauri taasisi binafsi kutumia fursa zilizopo katika maeneo mbalimbali, hususan mikoa ya Njombe, Ruvuma na Iringa ambako kuna vyanzo vingi vya maji vinavyoweza kutumika kuzalisha umeme, kuja kuwekeza ili kusaidia Serikali kuongeza upatikanaji wa nishati ya umeme nchini.
“Hatua hiyo itasaidia kuchochea shughuli za uchumi katika maeneo yatakayofikiwa na miradi hiyo kwani wananchi wataweza kujikwamua kiuchumi na kuwa na maendeleo” amesema.
Yesaya amesema mradi huo upo katika Kijiji cha Boimanda, Kata ya Matola, wilayani Njombe ambao unasimamiwa na Kanisa Katoliki Jimbo la Njombe kupitia Shirika la Benedictine Sisters of St. Gertrud Convent Imiliwaha.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi Sista Imakulata Mlowe, amesema kuwa mara baada ya mradi kukamilika, umeme utakaozalishwa utauzwa moja kwa moja kwa TANESCO ambapo tayari mkataba wa kuuziana umeme umeshasainiwa.
Ameongeza faida za mradi utakapokamilika utaongeza upatikanaji wa nishati ya uhakika kwa wananchi kwa matumizi ya nyumbani na biashara na kupinguza matumizi ya nishati isiyo rafiki na mazingira.
Ameeleza kuwa ujenzi wa mradi huo ulianza mwaka 2021 na baada ya miezi mitatu ijayo mtambo utawashwa na umeme kuingizwa katika Gridi ya Taifa.
Awali, Mratibu wa mradi huo, Sista Imakulata Mlowe, amesema utekelezaji wa mradi huo ulianza mwaka 2012, huku REA ikiwasaidia kuanzia hatua ya utafiti wa awali hadi hatua ya mwisho ya utekelezaji.
Aidha, amesema Tanesco ilitumia miundombinu iliyopo kuziunganishia huduma ya umeme kaya 212 zilizopo Boimanda.
Sista Imakulata amesema kazi iliyobaki ya kuunganisha miundombinu ya mradi itagharimu Sh bilioni 1.08 bilioni, na tayari maombi ya ruzuku yameshawasilishwa REA.
Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, amewahimiza Watanzania kuitumia fursa hiyo ya uwekezaji katika miradi ya uzalishaji umeme nchini badala ya kuiachia kwa wawekezaji wa kigeni.
“Masista hawa wameonesha njia kwa kuanzisha mradi huu. Vijana na wazee wamealikwa kuwekeza; tuitumie fursa hii vizuri,” amesema.








