Na Stella Aron, JamhuriMedia, Ludewa

Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), inatarajia kumaliza kilio cha wakazi wa vitongoji sita vilivyopo ukanda wa Ziwa Nyasa wilayani Ludewa, Mkoa wa Njombe, kwa kufikiwa na mradi wa kusambaza umeme uliogharimu sh bilioni 3.1.

Hayo yameelezwa leo Machi 12, 2026 na Msimamizi wa Miradi ya REA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Mhandisi Dastan Kalugira, wakati wa ziara ya wahariri ya kutembelea mradi wa kupeleka umeme katika vitongoji hivyo vilivyopo Ukanda wa Ziwa Nyasa wilayani na Ludewa mkoani Njombe.

‘Mradi huo upo Mkoa wa Njombe, lakini kuna vitongoji vinne vilivyopo ufukwe wa Matema wilayani Kyela mkoani Mbeya vimeunganishwa umeme kutoka upande huo kutokana na ugumu wa kuvifikia kupitia Njombe hata hivyo mradi huu ni wa kipekee kutokana na mazingira yake ya milimani” amesema.

“Changamoto kubwa ya ubebaji nguzo za umeme kuzisimika kwenye safu za milima Livingstone imechangia ugumu wa kufikia vitongoji ambavyo vilikuwa gizani sasa vitapata umeme hata hivyo tunashukuru utekelezaji wake umefanikiwa kutokana na uwezeshwaji mkubwa uliofanywa na REA” amesema.

Amesema mkandarasi anayetekeleza mradi huo ni Suma JKT ambaye tayari amekamilisha kazi ya kusimamisha nguzo zote 105 zinazohitajika kwa mradi huo na hatua iliyobaki ni kuvuta waya ili kukamilisha miundombinu ya usambazaji wa umeme kabla ya wananchi kuanza kupata huduma hiyo.

Amesema kuwa mradi huo utanufaisha kaya za awali takribani 160, huku Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) likitarajiwa kuendelea kuwaunganisha wateja wengine wapya kwa gharama za REA baada ya kukamilika kwake.

Aidha vitongoji vitakavyonufaika na mradi huo ni Kitewele na Kimata vilivyopo wilayani Ludewa, pamoja na Kigulu, Chanjale, Lumbira na Nkanda vilivyopo upande wa Matema wilayani Kyela.

Kwa upande wake, Msimamizi wa mradi huo kutoka SUMA JKT, Yassin Seleman, amesema mradi huo upo katika Kijiji cha Madunda, Kata ya Mawengi, wilayani Ludewa,mkoani Njombe.

Amesema licha ya changamoto walizokutana nazo wakati wa utekelezaji ikiwemo mvua iliwalazimu kusafirisha nguzo moja kwa siku kwenda eneo la mradi kwa kutumia trekta kutokana na ugumu kufika kqenye milima.

Ameongeza kuwa utekelezaji wa mradi huo pia umechangia kutoa ajira kwa wananchi 80 wakati wa kipindi cha utekelezaji wake.


Kwa mujibu wa takwimu za Mkoa wa Njombe, kuna jumla ya Vijiji 381 ambapo vyote tayari vimeunganishwa na huduma ya umeme.

Kati ya vitongoji 1,833 vilivyopo mkoani humo, vitongoji 1,249 tayari vimepata umeme huku vitongoji 584 vikiwa mbioni kufikiwa na huduma hiyo.

Naye Mwenyekiti Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile amesema miradi ya kusambaza umeme vijijini inayotekelezwa na inaonesha wazi namna makato ya asilimia tatu ya ununuzi wa umeme yanavyotumika kuleta maendeleo kwa wananchi.

Balile amesema kuwa miradi hiyo ni ushahidi kuwa michango ya wananchi kupitia makato hayo inarejea kwa jamii kwa kugharamia miradi ya maendeleo.

“Leo tumeshuhudia vitongoji sita vilivyopo katika mazingira magumu vikielekea kupata huduma ya umeme. Hii inaonesha wazi kuwa ile asilimia tatu inayokatwa kila tunaponunua umeme kupitia REA inafanya kazi,” alisema Balile.

Ameongeza kuwa hakuna maendeleo yanayoweza kupatikana bila wananchi kushiriki kugharamia miradi ya maendeleo.

“Hakuna mahali tunaweza kupiga hatua bila kugharamia maendeleo yetu wenyewe. Ni lazima tuchangie maendeleo ili nchi yetu ipige hatua hata bila kusubiri wafadhili,” alisema.

Mradi huo wa kusambaza umeme katika vitongoji sita unatekelezwa na REA kwa gharama ya shilingi bilioni 3.1 na ulianza kutekelezwa Julai 13, 2025 huku ukitarajiwa kukamilika Aprili 13, 2026.