Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Zanzibar
Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Dkt. Mohamed Said Dimwa, ameitaka Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) kuendeleza utamaduni wa kuwajengea uwezo wa kitaaluma na kiuongozi vijana ili kuandaa kizazi cha viongozi na watendaji bora wa sasa na baadaye.
Dkt. Dimwa aliyasema hayo wakati akizungumza katika iftar iliyoandaliwa na UVCCM Zanzibar na kufanyika katika Chuo Cha Mafunzo na Uongozi cha UVCCM Tunguu, Zanzibar, ikiwa ni sehemu ya shughuli za kijamii katika mwezi mtukufu wa Ramadhan.
Katika hotuba yake, Dkt. Dimwa alieleza kuwa chama hicho kimejipanga kuhakikisha mpango wa kuwajengea vijana uwezo wa kitaaluma na uongozi unakuwa endelevu na unasimamiwa kikamilifu na CCM ili kuwafikia vijana wa makundi mbalimbali nchini.
Alisema lengo la mpango huo ni kupata vijana imara wenye uwezo wa kukabili changamoto za jamii, ikiwemo tatizo la ajira, pamoja na kuwaandaa viongozi na watendaji wenye uzalendo, uaminifu na uchapakazi katika taasisi mbalimbali za umma na binafsi.

Aidha, alibainisha kuwa mafunzo hayo yataenda sambamba na programu za mafunzo ya amali na ujasiriamali ili kuwawezesha vijana kujiajiri kulingana na fursa zilizopo katika mazingira wanayoishi.
“CCM imeendelea kuwa chama kiongozi na mfano bora katika kuandaa viongozi wenye uwezo wa kuongoza kwa ufanisi katika ngazi mbalimbali za kitaifa na kimataifa,” alisema Dkt. Dimwa.
Katika hatua nyingine, aliipongeza UVCCM kwa kuandaa iftar hiyo iliyowakutanisha vijana na wanachama mbalimbali wa chama hicho, akisema ni sehemu ya kudumisha umoja, mshikamano na upendo ndani ya chama na jumuiya zake.
Dkt.Dimwa Alisema, dhamira ya CCM ni kuhakikisha vijana wake wanajifunza na kubadilishana uzoefu na vijana wa vyama vingine vikiwemo vyama vya ukombozi Kusini mwa Afrika vya ANC (Afrika Kusini), MPLA (Angola), SWAPO (Namibia), ZANU PF (Zimbabwe), FRELIMO (Msumbiji) na Chama Cha Kikomunisti cha China(CPC).
Amesisitiza umuhimu wa UVCCM kwenda na wakati wa sasa wa soko la ajira na uongozi linalohitaji vijana walioiva na wenye uwezo wa kitaaluma sambamba na ujuzi wa fani zinazoendana na mahitaji ya zama za Sayansi na Teklojia.
Alisema mwezi mtukufu wa Ramadhan ni wakati muhimu wa ibada na kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu, hivyo aliwasihi waumini kuutumia kufanya toba, kujiepusha na maovu na kuimarisha maadili mema katika jamii.

Pia alitoa pongezi kwa Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kusimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM tangu walipoingia madarakani kufuatia uchaguzi mkuu uliopita.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi Taifa, Mohamed Kawaida, aliahidi kuwa jumuiya hiyo itayafanyia kazi kwa haraka maelekezo yaliyotolewa na Dkt. Dimwa, akisema UVCCM inaendelea kujiimarisha kupitia mipango endelevu ya mafunzo ya ujuzi na maarifa kwa vijana.
Alisema lengo la UVCCM ni kuhakikisha vijana wanakuwa wabunifu na wenye uwezo wa kutumia fursa zinazowazunguka ili kujiongezea kipato na kuchangia maendeleo ya taifa.
“Lengo letu ni kuhakikisha jumuiya yetu inakuwa na vijana wenye fani mbalimbali na viwango vya elimu ya juu, wanaoweza kuaminiwa kuwa viongozi katika taasisi mbalimbali ndani na nje ya nchi, lakini wakiwa na uzalendo na dhamira ya kuwatumikia wananchi kwa ufanisi,” alisema Kawaida.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar, Abdi Mahmoud Abdi, alisema jumuiya hiyo itaendelea kuwaandaa vijana wake ili wawe imara katika nyanja za uongozi, utendaji, ubunifu na uchapakazi.
Abdi aliwashukuru viongozi na wanachama wote waliohudhuria iftar hiyo, huku akiwahimiza kuendelea kufanya ibada na kutenda mema katika kipindi chote cha mwezi mtukufu wa Ramadhan.


