Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kibaha

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya TAMISEMI imeielekeza Serikali kuongeza fedha ili kukamilisha ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami ya Pichandege–Sofu–Bokomnemela kutokana na umuhimu wake katika kurahisisha usafiri wa wananchi kuelekea Stesheni ya SGR.

Pia imeitaka Serikali kuongeza fedha kwa ajili ya kukamilisha mradi wa ujenzi wa barabara ya Kongowe–Forest–Yombo yenye urefu wa mita 700 (sawa na kilometa 0.7), ambayo ni kiungo muhimu cha ukuaji wa uchumi na inayorahisisha usafiri kuelekea Bagamoyo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya TAMISEMI, Florent Kyombo, alitoa maelekezo hayo baada ya kamati hiyo kukagua miradi hiyo miwili ya barabara iliyo chini ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Machi 14, 2026.

Alieleza ,barabara ya Pichandege–Sofu–Bokomnemela ni muhimu kwani itarahisisha wananchi wa Mkoa wa Pwani kufika Stesheni ya SGR bila kulazimika kupitia Dar es Salaam ambako ni umbali mrefu.

“Pia barabara ya Kongowe–Forest itasaidia kurahisisha usafiri kuelekea Bandari ya Bagamoyo, kufungua fursa za maendeleo na kuwaondolea adha wananchi wa maeneo ambayo bado barabara haijakamilika,” alieleza Kyombo.

Naibu Waziri wa TAMISEMI, Dkt. Jafar Seif, alieleza wamepokea maelekezo ya kamati hiyo na kusisitiza kuwa wanaendelea kusimamia miradi hiyo ili kuhakikisha vipande vilivyobakia vinakamilishwa kwa wakati na kurahisisha usafiri kwa wananchi.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini, Silvestry Koka, aliishukuru Serikali kwa kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya miradi ya barabara katika Manispaa ya Kibaha.

Alisema lengo ni kuhakikisha barabara zinajengwa kwa ubora unaolingana na fedha zilizotengwa ili kuleta manufaa kwa wananchi, sambamba na dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuboresha miundombinu na kuleta tabasamu kwa Watanzania.

Diwani wa Kata ya Sofu, Mashaka Mahande, aliomba Serikali iitazame kwa jicho la tatu barabara ya Sofu ambayo ni kiunganishi muhimu kuelekea Stesheni ya SGR na Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Nelson Mandela (TNG) ambacho kitahudumia wanafunzi kutoka ndani na nje ya nchi.

Meneja wa TARURA Mkoa wa Pwani, Ibrahim Kibasa, alieleza barabara ya Sofu–Bokomnemela imepata fedha kwa awamu nne kwa ajili ya utekelezaji wake.

Alielezea kuwa, mradi huo unatekelezwa na mkandarasi M/S Old South Co. Ltd wa Kibaha, ambapo utekelezaji ulianza Agosti 2024 na unatarajiwa kukamilika Machi 2026 ukiwa umefikia asilimia 95, hadi sasa mkandarasi amelipwa Sh milioni 273,928,200 kwa kazi iliyotekelezwa.

Kadhalika, mradi wa barabara ya Kongowe–Forest–Bagamoyo wenye urefu wa mita 700 umefikia asilimia 95 ya utekelezaji, ukiwa na mkataba wa Sh milioni 760, ambapo hadi sasa mkandarasi amelipwa Sh milioni 661,849,315.

Baadhi ya wananchi wa Kongowe akiwemo Brian Malik, Denis Desideri na Issa Komba waliishukuru Serikali kwa mpango wa kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami na kuiomba TARURA kuongeza kasi ya kumalizia kipande kilichobakia ili kuondoa changamoto ya barabara mbovu katika eneo la Forest ambako lami bado haijafika.