Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa amewaomba msamaha wananchama na viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kufuatia kauli yake aliyoitoa wakati akiwa katika halfa ya chakula katika Ikulu Ndogo mkoani Iringa.

Katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na Rais Dkt Magufuli na viongozi waandamizi wa serikali ya awamu ya tano na viongozi wengine wastaafu, Msigwa ambaye ni Mbunge wa upinzani wakati akizungumza aliipongeza serikali kwa namna ambavyo imekuwa ikitoa fedha za miradi ya maendeleo pamoja na ukarabati wa barabara tangu ilipoingia madarakani.

Msigwa alisema kuwa, serikali iliyo chini ya Rais Dkt Magufuli haina upendeleo na kwamba hata maeneo yanayoongozwa na upinzani yanapata maendeleo sawa na yale yaliyochini ya chama tawala, na kusema kuwa, kauli ya Rais kwamba maendeleo hayana chama imedhihirika kwa vitendo.

Kufuatia hatua hiyo, watu mbalimbali wamemkosoa Mchungaji Msigwa kwa kudai kuwa amekwenda kinyume na aliyokuwa akiyazungumza hadharani na kwenye mitandao ya kijamii, kwani amekuwa akikosoa utendaji wa awamu ya tano, na hivyo wameshangaa imekuaje ghafla amebadilika na kuipongeza.

Mbali na kutoa ufafanuzi wa kauli yake, watu wengi walionekana kutokumuelewa na hivyo Msigwa akalazimika kuomba msamaha kwa viongozi na wananchama wa chama hicho, huku akiwataka kuendelea na mapambano badala ya kuhangaika na jambo dogo alilokosea.

“Ufafanuzi wangu bado haueleweki na ni heshima kuzingatia maumivu yenu kwa mkanganyiko huu. Nagundua rafiki zangu na wanachama wetu wanaugua.Basi niseme nini?Naomba nisameheni sana. The cause we are fighting for is more important than my personality. I take full responsibility,” ameandika Mchungaji Msigwa.

Mbali na waliomkosoa Msigwa, wapo baadhi walioungana naye na kusema kuwa, ingekuwa vigumu kwake kuikosoa serikali kwa mazingira aliyokuwapo, na hivyo wanaona alichofanya kilikuwa ni sahihi. Pia wameeleza kwamba, mbali na mapungufu ya serikali, lakini ni lazima ikubalike kuwa, kuna mambo ambayo inafanya vizuri, yakiwamo ambayo Mchungaji Msigwa aliyataja.

Mchungaji Msigwa alisema, wapo wanaoamini kwamba anaunga mkono kila kitu kinachofanya na serikali, lakini kwake si kweli, na kwamba ataendelea kuikosoa serikali ili itekeleze wajibu wake.

 

By Jamhuri