Na Eleuteri Mangi, JamhuriMedia, Kilimanjaro

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeridhishwa na kazi ya uimarishaji wa mpaka wa Kimataifa kati ya Tanzania na Kenya ambapo Km 564 sawa asilimia 75 tayari zimewekewa alama kati ya km 758 za mpaka mzima wa nchi kavu.

Akizungumza wakati wa ziara ya kamati hiyo eneo la Holili, wilayani Rombo Mkoa wa Kilimanjaro, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Timotheo Mzava amesema kazi ya kuweka alama kwenye mipaka sio kazi ndogo na kuipongeza Wizara ya Ardhi kwa kazi kubwa iliyofanya.

“Kipekee kwenye mpaka huu, ukisimama hapa unaona mpaka kule juu unaona alama zimewekwa, hii ni kazi kubwa imefanyika, nawapongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kazi kubwa ambayo mmeifanya”, amesema Mzava.

Aidha, Kamati imeitaka Serikali kukamilisha kazi ya uimarishaji mpaka huo wa kimataifa kati ya Tanzania na Kenya huku ikitarajia kuona mipango ya kifedha na bajeti inayoonesha mwelekeo na nia ya dhati ya kukamilisha kazi hiyo kwenye bajeti ya sasa na inayokuja katika mwaka wa fedha 2026/2027.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Kaspar Mmuya amewataka wataalamu wa Wizara ya Ardhi kuendelea kutoa elimu kwa wananachi wa maeneo ya mipakani kwa lugha ile ile ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili waelewe na kuwa sehemu ya ulinzi wa mipaka ya nchi.

“Dhana kubwa hata kwenye Katiba ya nchi inasema, hata mwananchi mwenyewe ana dhamana ya kulinda mipaka ya nchi yake, ndiyo maana unapofanya kazi ya uimarishaji wa mipaka na ukiishi kwenye mipaka hii tunawahusisha wananchi kwa kutoa elimu kuwa wana dhamana ya kuilinda mipaka ya nchi yao”, amesisitiza Naibu Waziri Mmuya.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Rombo Raymond Mwangwala ameiambia kamati hiyo ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii kuwa mpaka wa nchi hizo mbili uko salama na wananchi wanaendelea na shughuli zao za kiuchumi na wana uhusiano mzuri na kuweka wazi kuwa wote walishiriki vizuri kwenye zoezi la kuweka alama kwenye mipaka.

Mpaka wa Tanzania na Kenya umekuwa ni eneo la mfano wa kuigwa kwenye ukanda wa Afrika kwa mujibu wa Taasisi ya Uimarishaji wa Mipaka Afrika inayojulikana kama African Union Border Program.