Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Denis Londo amesema Serikali itaendelea kuimarisha uwekezaji katika elimu ya juu ili kuwajengea vijana uwezo wa kushindana katika soko la ajira ndani na nje ya nchi.

Akizungumza jijini Dar es Salaam katika futari iliyoandaliwa na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu kwa wadau wake, alisema mafanikio ya bodi hiyo yanaonesha dhamira ya Serikali katika kusaidia vijana wengi kupata elimu ya juu.

Londo alisema chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, Serikali imeendelea kuongeza fedha za mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu ili kuwapa fursa zaidi vijana kufikia ndoto zao za kitaaluma.

“Ongezeko hilo la fedha limewezesha idadi ya wanufaika kuongezeka kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na miaka iliyopita, jambo linalodhihirisha dhamira ya Serikali kuwekeza katika rasilimali watu”,Amesema Londo.

Akizungumzia teknolojia alisema maendeleo ya teknolojia yameboresha huduma za bodi hiyo, kwani sasa wanafunzi wanaweza kuomba mikopo wakiwa vijijini bila kulazimika kusafiri hadi mijini, hali inayopunguza gharama kwa wazazi na wanafunzi.

Aidha Naibu waziri huyo alisisitiza kuwa uwekezaji katika elimu ni uwekezaji katika mustakabali wa taifa, kwani taifa linalowekeza kwa vijana wake linajiandaa kuwa na wataalamu watakaolisukuma mbele maendeleo.

Sambamba na hayo aliwataka wanufaika wa mikopo hiyo kutambua kuwa fedha wanazopata ni mkopo unaopaswa kurejeshwa ili kuwapa nafasi vijana wengine kunufaika na programu hiyo.

“Yeyote aliyenufaika na mkopo na akapata ajira au kipato anapaswa kurejesha fedha hizo kwa uaminifu, kwani kufanya kinyume chake ni kuwanyima nafasi vijana wengine wanaotamani kusoma,” alisema.

Akizungumzia mwezi mtukufu wa Ramadhani, alisema ni kipindi muhimu cha ibada, kutafakari na kuimarisha mshikamano miongoni mwa jamii huku akipongeza uongozi wa bodi hiyo kwa kuandaa tukio hilo ambalo limewakutanisha wadau mbalimbali wanaoshirikiana katika kusaidia maendeleo ya elimu nchini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) Dkt Bill Kiwia alitoa wito kwa taasisi za umma na binafsi kushirikiana na bodi hiyo katika kusaidia kufadhili masomo ya vijana wenye uhitaji ili kuongeza idadi ya Watanzania wanaopata elimu ya juu na kutimiza ndoto zao.