Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kibaha
MKURUGENZI wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Ladslaus Mnyone, amewataka viongozi wa taasisi mbalimbali kuwa wabunifu na kuonesha uongozi bora katika kutekeleza majukumu yao ili kusaidia kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Aidha, amewaasa viongozi kujiamini, kujenga utamaduni wa kuibua viongozi wengine pamoja na kuimarisha ushirikiano mahali pa kazi, huku akikemea tabia ya kufanya kazi kwa mazoea.
Mnyone ametoa wito huo wakati akifunga mafunzo ya siku nne ya uongozi kwa viongozi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) yaliyofanyika katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere, Kwamfipa mkoani Pwani.
Amesema viongozi wanapaswa kutumia maarifa waliyopata katika mafunzo hayo, ikiwemo matumizi ya akili hisia (emotional intelligence), katika kuboresha utendaji wao, kutatua changamoto kwa ubunifu na kusimamia ipasavyo rasilimali watu na fedha ili kuinua maendeleo ya taasisi na taifa kwa ujumla.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Profesa Alex Makulilo, amesema mafunzo hayo ni ya kimkakati kwa kuwa yanalenga kuwajengea viongozi mabadiliko ya kifikra yatakayosaidia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Ameongeza kuwa chuo hicho tayari kimeandaa mpango kazi wa miaka mitano unaolenga kuakisi dira hiyo, akisisitiza kuwa uongozi bora ni msingi muhimu katika kufanikisha malengo ya maendeleo ya taifa.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere, Profesa Marcellina Chijoriga, Meneja Taaluma John Baitan amesema mafunzo hayo yaliyofanyika kuanzia Machi 11 hadi 14, 2026 yalihusisha washiriki 75 kutoka OUT na yalilenga kuwajengea uwezo viongozi hao ili kuongeza ufanisi katika utendaji wao.
Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kilianzishwa mwaka 1992 kwa Sheria ya Bunge Na. 17 kwa lengo la kupanua upatikanaji wa elimu ya juu kwa Watanzania kupitia mfumo wa elimu ya masafa.





