Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kibaha
SERIKALI kupitia Wizara ya Kilimo imeanza hatua za kuanzisha shamba maalum la mbogamboga Ruvu, wilayani Kibaha ,mkoani Pwani, lengo likiwa kuongeza uzalishaji wa mazao hayo ili kukidhi mahitaji ya chakula na lishe kwa Watanzania katika miji ya Dar es Salaam na Zanzibar, huku ikifungua fursa za masoko ya ndani na nje ya nchi.
Hatua hiyo inalenga kutafsiri kwa vitendo dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuimarisha sekta ya kilimo, kuboresha lishe ya wananchi na kuhakikisha nchi inajitosheleza kwa chakula, huku Tanzania ikiwa na uwezo wa kulisha hata mataifa mengine ya Afrika.
Akiwa ameambatana na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, Mkuu wa Wilaya ya Kibaha pamoja na wataalamu wa taasisi za kilimo na umwagiliaji kwa ajili ya tathmini ya eneo hilo Machi 16, 2026, Waziri wa Kilimo Daniel Godfrey Chongolo amesema lengo kubwa ni kuanzisha mashamba darasa ya mfano kwa kilimo cha mbogamboga.
Chongolo alieleza, ingawa baadhi ya wakulima katika mkoa huo tayari wanafanya kilimo hicho, uzalishaji bado ni mdogo ukilinganishwa na mahitaji makubwa yaliyopo Pwani, Dar es Salaam na Zanzibar, hasa kutokana na idadi kubwa ya wakazi na watalii wanaotembelea visiwa hivyo.
“Tumepewa dhamana na Rais kuhakikisha Wizara ya Kilimo inafanikiwa kulisha Watanzania na wengine kibiashara, katika eneo la mboga na matunda saidizi bado hatujawekeza nguvu kubwa,” alifafanua Chongolo.
Alieleza katika hatua ya kwanza mradi huo utaanza na hekari 200, huku akisisitiza kuwa taratibu zote zikikamilika mwezi Juni mwaka huu uzalishaji uanze ili kuleta matokeo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge alieleza, mradi huo unatarajiwa kuongeza ajira kwa wananchi hususan vijana.
Kadhalika ,serikali imeshanunua mabehewa maalum manane kupitia reli ya kisasa ya SGR kwa ajili ya kusafirisha mbogamboga kutoka maeneo ya uzalishaji kwenda katika masoko makubwa hivyo itawezesha kupunguza upotevu wa mazao.
Kunenge alibainisha kuwa, hatua hiyo inaendana na malengo ya Dira ya Maendeleo 2050 na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi inayolenga kuzalisha ajira milioni nane nchini, huku akisisitiza kuwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan pia ni kinara wa kimataifa katika kuhamasisha lishe bora na kupunguza vifo vya mama na mtoto.








