Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Zanzibar

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweka mazingira rafiki katika sekta binafsi kwa lengo la kuimarisha vivutio vya uwekezaji, kukuza ushirikiano kupitia ubia wa sekta ya umma na binafsi (PPP) katika miradi ya kimkakati.

Akizungumza na waandishi wa habari katika nukumbi wa Idara ya Habari Maelezo kuhusiana na siku 100 za mafanikio ya uongozi wa DK. Mwinyi, Waziri wa Kazi na Uwekezaji Mhe. Shariff Ali Shariff amesema Serikali imetekeleza miradi ya kimkakati ikiwemo miundombinu, nishati mbadala na huduma za kijamii ili kuimarisha uchumi na ukuaji wa nchi.Aidha amesema Serikali inaendelea kuratibu programu za kusimamia usalama na afya kazini, utekelezaji wa viwango vya kazi ili kulinda maslahi ya wafanyakazi ikiwemo mikataba, mishahara, saa za kazi na stahiki za wafanyakazi.

“Kuimarisha usimamizi wa usuluhishishi wa utatuzi wa migogoro ya kazi kwa lengo la kukuza mahusiano mema ya kazi baina ya waajiri na waajiriwa pia kuendelea kusimamia utaratibu maalumu wa kazi kwa wageni kwa kufanya kazi katika miradi ya maendeleo hapa nchini”Waziri Shariff ameeleza kuwa Serikali inaendelea ujenzi wa miundombinu katika maeneo huru ya uwekezaji ambapo Mamlaka imefanya zoezi la ukaguzi na tathmini kwa ajili ya ulipaji fidia katika maeneo makuu matatu ambapo ni tathmini ya upanuzi katika eneo la bandari ya Fumba, ujenzi wa km 8 za barabara za ndani katika eneo la uwekezaji Fumba pamoja na eneo la mradi wa IT Madrasa.

“Serikali imesajili miradi ya uwekezaji 45 yenye thamani ya dola za kimarekani 218,037,508 na kufikia jumla ya miradi 607 yenye thamani ya dola za kimarekani 6.9 bilioni , katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Nane kufanya miradi yote iliyosajiliwa na ZIPA kufikia miradi zaidi ya 1,351 yenye thamani ya zaidi ya dola za kimarekani 14.4 bilioni” amefahamisha.

Akizungumzia sekta ya kazi, amesema Serikali inaendelea kuhakikisha haki na maslahi ya wafanyakazi yanalindwa kwa kufanya ukaguzi katika taasisi 78 Unguja na Pemba, ukaguzi huo umebaini kuwa asilimia 95 ya taasisi hizo zinalipa kima cha chini cha mshahara kisichopungua shilingi 347,000 kwa mwezi, sambamba na kuzingatia sheria za kazi kuhusu saa za kazi na malipo ya muda wa ziada.

Kwa upande wa sekta ya kazi, amefahamisha kuwa Kamisheni ya Kazi imefanya ukaguzi wa kawaida kwa Taasisi 78 Unguja na Pemba kwa lengo la kuhakikisha taasisi hizo zinatekeleza Sheria za kazi katika kulinda haki na Maslahi ya wafanyakazi.

“Ukaguzi huo ulihusisha kuangalia utekelezaji wa malipo ya kima cha chini cha mshahara ambapo asilimia 95 ya taasisi zilizokaguliwa zimeonekana wanalipa kima kisichopungua TZS 347,000/=, pia imeonekanwa kuwa saa za kazi na viwango vya malipo ya muda wa saa za ziada, pamoja na stahiki za wafanyakazi zinazingatiwa kwa mujibu wa Sheria”.

Mhe. Sheriff amefahamisha Serikali ipo katika hatua ya kufanya tathmini ya kima cha chini cha mshahara kilichopo kwa sasa katika sekta binafsi ambacho kilitangazwa mwaka 2023 kwa lengo la kuangalia uhalisia wake kulingana na mabadiliko ya hali ya uchumi.

“Tunaangalia gharama za maisha pamoja na mazingira ya soko la ajira ili kuhakikisha kiwango hicho kinaendelea kuwa stahiki na chenye kulinda maslahi ya wafanyakazi bila kuathiri ukuaji wa sekta binafsi” amefahamisha Waziri Shariff.