Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umewapa mafunzo waajiri 129 wa sekta binafsi, yakilenga kuwaongezea uelewa wa kina kuhusu utekelezaji sahihi wa sheria za hifadhi ya jamii na matumizi ya mifumo ya kidijitali katika kurahisisha huduma.
Akizungumza kwenye mkutano ulioandaliwa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Meneja wa Uandikishaji, Ukaguzi na Matekelezo wa NSSF, Bw. Cosmas Sasi, alisema ushirikiano kati ya Mfuko na Chama hicho umeendelea kuzaa matunda kwa kuwajengea uwezo waajiri katika kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
“Lengo letu ni kuhakikisha mwajiri anatekeleza sheria ya NSSF kwa uelewa, si kwa kulazimishwa. Ndiyo maana tunaendelea kutoa elimu ili wajue wajibu wao kikamilifu,” alisema Bw. Sasi.
Alieleza kuwa mafunzo hayo yalijikita katika masuala muhimu, ikiwemo usajili wa waajiri na wafanyakazi, pamoja na uwasilishaji wa michango kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa kisheria.

Bw. Sasi alisisitiza kuwa uwasilishaji wa michango kwa wakati ni nguzo muhimu katika kuhakikisha wafanyakazi wanapata mafao yao bila vikwazo wanapoyahitaji.
Katika hatua nyingine, aliwahimiza waajiri kutumia kikamilifu Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), akibainisha maboresho yaliyofanyika kwenye mfumo wa NSSF Portal unaowezesha utekelezaji wa huduma mbalimbali kwa njia ya mtandao.
Kupitia mfumo huo, waajiri wanaweza kujisajili, kusajili wafanyakazi, kuwasilisha michango, kufanya ukaguzi, pamoja na kuomba semina kwa ajili ya wafanyakazi wao.
“Tumeboresha mifumo yetu ili kumrahisishia mwajiri kutekeleza majukumu yake kwa haraka na kwa ufanisi zaidi,” aliongeza Bw. Sasi.
Aidha, waajiri walielimishwa kuhusu namna ya kufungua madai mtandaoni pamoja na wajibu wao wa kuhakiki taarifa za wafanyakazi wanaowasilisha madai hayo.

Pia walipatiwa ufafanuzi kuhusu mfumo mpya wa uhakiki wa wastaafu unaofanyika kidijitali, hatua inayookoa muda na kurahisisha huduma.
Bw. Sasi aliwataka waajiri kuendelea kushirikiana na NSSF kwa kuhakikisha wafanyakazi wote wanasajiliwa na michango yao inawasilishwa kwa wakati.
Kwa upande wao, baadhi ya waajiri walieleza kuridhishwa na huduma za NSSF. Mariam Issa alisema Mfuko huo umekuwa msaada mkubwa kwa wafanyakazi, akitoa mfano wa mfanyakazi wao aliyenufaika na matibabu hadi akapona.
Naye, James Bidianguze aliipongeza NSSF kwa huduma bora, akibainisha kuwa mafao ya matibabu yanayotolewa na Mfuko yamekuwa mkombozi kwa wafanyakazi wengi wa sekta binafsi.
Mafunzo hayo yameongeza uelewa kwa waajiri na kuimarisha ushirikiano na NSSF katika kuhakikisha utekelezaji bora wa sheria za hifadhi ya jamii nchini.





