Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Tume ya Rais ya Kutathmini Maboresho ya Mfumo wa Kodi Nchini, chini ya Balozi Ombeni Sefue, imewasilisha ripoti yake kwa Rais Samia Suluhu Hassan wiki iliyopita. Tume imekuja na mapendekezo 284. Si madogo, yanaashiria ukubwa wa tatizo. Mapendekezo haya yametokana na maoni yaliyotolewa na walipa kodi, ambao maisha yao ni magumu. Walipakodi tulio wengi, tunaishi katikati ya moto na kikaango.
Sitanii, kwa nini nasema tunaishi katikati ya kikaango na moto? Ukiacha wafanyakazi wa serikali, ambao wao wanafahamu siku yao ya kulipwa posho na mishahara, na kimsingi nisamehewe niseme wazi kuwa hawa siwahesabu kama walipakodi. Najua utashangaa, msomaji, kuwa mbona wanalipa kodi inayoitwa Lipa Kadri Unavyopata (PAYE), wanalipa kodi ya ujuzi (SDL) na mimi leo nazomokaje kusema hawalipi kodi wao kama mfanyakazi wa serikali au watumishi wa kisiasa ambao mafao yao yanatokana na ruzuku ya vyama au Hazina?
Namaanisha. Wasimamizi wa kodi wengi, iwe ni katika ngazi ya watendaji au watunga sera, wengi wao hawajawahi kufanya biashara na hawajawahi hata kufuga kuku. Hawajui kuwa hata hiyo mishahara wanayolipwa kama watumishi wa umma inatokana na fedha za wafanyabiashara, wakulima, wafugaji, wachimba madini, watoa huduma za usafiri, usafirishaji na makundi mengine ambayo lazima uuze kitu, upate fedha, kisha ulipe kodi.
Watumishi wa umma, nafahamu mtasema mnauza ujuzi kutupatia huduma. Silipingi hili, lakini ninyi mna uhakika. Mkiuza ujuzi wenu katika taasisi mbalimbali, makusanyo yanayotokana na kazi ya mikono yetu kama wafanyabiashara yanakuwa tayari yapo Hazina. Mgawo unatoka unaingia katika akaunti zenu kama mishahara au taasisi mnazoziendesha kama OC (matumizi ya kawaida), maisha yanasonga.

Sitanii na msinichukie, ngoja niwambie ukweli mchungu. Wanasiasa wengi na baadhi ya watumishi wa umma wanakuwa kama mashabiki wa Simba na Yanga. Simba akifungwa na Pamba kwa goli la adhabu ndogo inayopigwa moja kwa moja, kipa analaumiwa kuwa hakusimama katikati ya milingoti. Mtibwa akipiga kona, golikipa wa Yanga akawa anasukumana na mshambuliaji wa Mtibwa, kona ikaingia moja kwa moja, tunaingia kwenye mjadala wa golikipa hakuwa makini.
Waswahili wanasema ukitaka kujua uhondo wa ngoma, uingie ucheze. Naomba nifungue kabrasha kidogo. Sheria ya Kodi ya Mapato, Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na kodi nyingine nyingi, uhusiano wake kati ya mlipakodi (mfanyabiashara) na mtoza kodi ni sawa na polisi na mhalifu. Wazo kuu muda wote katika sheria hizi ni kuwa walipakodi ni wakwepaji, hivyo ikifika muda wa kulipa kodi, walipe tu. Wanazitoa wapi na walipaje, haliwahusu.
Nimeziona ishara na natamani Rais Samia Suluhu Hassan ageuze mtazamo huu, uhusiano kati ya mlipisha kodi na mlipa kodi uwe sawa na nesi/daktari na mgonjwa. Hakuna daktari anayempa mgonjwa dawa bila kufahamu historia ya ugonjwa wake. Ikifanyika hivyo, matokeo yanafahamika. Mtu atapewa dawa ya tumbo ilhali anaumwa kichwa na mwisho wa utaratibu huu wa daktari kumwandikia dawa mgonjwa bila kumsikiliza na kuchunguza, kisha kumwandikia dawa (diagnosis and prescription), ni kifo.
Kwa bahati mbaya hili halipo kwa wakusanya kodi. Sisi walipakodi hatuna tofauti na mgonjwa. Tofauti yetu ni kuwa mgonjwa amelazwa hospitalini na sisi tupo ofisini. Naomba niwashirikishe. Nitatumia mfano wa vyombo vya habari nilipofanya uwekezaji. Nikizungumza na wawekezaji katika sekta nyingine, nao wananiambia hayo hayo.
Sitanii, leo unaweza kujikuta kampuni yako inadai serikalini na taasisi mbalimbali walau Sh milioni 700. Lakini huna fedha ya uchapaji Sh milioni 8 au kulipa mishahara, ambayo si mikubwa kama wakubwa wanaolipwa hadi milioni 40, bali milioni 21 kwa waajiriwa 25. Unaweza kujiuliza inakuwaje? Nitatoa jibu si muda. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wao wanakusanya kodi.
TRA wamewekewa na serikali kupitia bungeni tarehe mahususi za kulipa kodi. Kila ikifika tarehe saba ya mwezi mpya unapaswa kuwa umewasilisha marejesho (returns) za PAYE na SDL. Tarehe 20 ya mwezi unaofuata unawasilisha marejesho ya VAT. Ukiwasilisha haya marejesho unapewa hati ya malipo ambayo chini yake imeandikwa kuwa kama hukubaliani na kiwango cha kodi husika, basi uipinge kodi hiyo ndani ya siku 30.

Haya ni maandishi tu. Ikifika tarehe 8 ya mwezi mpya kwa PAYE na SDL au tarehe 21 ya mwezi mpya kwa kodi ya VAT na mwisho tarehe ya kwanza ya mwisho wa robo yoyote ya mwaka kwa kodi ya makadirio (presumptive), kwa mikoa yenye mameneja wa mikoa ya kikodi, waungwana watu wake wanakupigia simu kukumbia kuwa hujalipa kodi husika.

Mameneja ‘kauzu’, wanakuandikia barua kuwa umegoma (default) kulipa kodi siku moja baada ya tarehe ya marejesho. Bila kujali kuwa kuna siku 30 za kuipinga kodi husika katika hati ya marejesho uliyopewa. Wababe zaidi kabla ya ujio wa Rais Samia Suluhu Hassan walikuwa wanatoa hati ya uwakala wa kukusanya kodi kwa benki (agency notice) chini ya kifungu cha 67 cha Sheria ya Usimamizi wa Kodi. Hii Tume ya Jaji Ombeni imesema itolewe baada ya hukumu ya kimahakama. Safi.
Ikishatolewa hiyo hati ya uwakala, fedha zinaruhusiwa kuingia tu kwenye akaunti, bila kutolewa. Kwa hiyo zikitimia kiwango ambacho wababe hao wamesema wanakudai, zinachukuliwa kwenda TRA. Hapa hawafanyi kama afanyavyo daktari na mgonjwa. Hawakuulizi kwa nini umeshindwa kulipa kodi. Lakini nilitarajia swali hili lije baada ya kupita siku 30 tangu ulipowasilisha marejesho. Ila hili haliko hivyo kisheria.
Sitanii, msomaji, ujue mpaka hapo sijakwambia kwa nini tunashindwa kulipa kodi kwa wakati. Sheria za kodi zinasema unapouza bidhaa toa risiti. Mfano mimi kwenye gazeti langu la JAMHURI tunapouza matangazo tunapaswa kutoa risiti ya EFD kabla ya kulipwa. Rudia, kabla ya kulipwa. Ukitoa risiti, hivyo inageuka kodi. TRA hawajui kama umeishalipwa au la.
Kwa kuwa katika Sheria ya Huduma za Habari ya Mwaka 2016 kifungu cha 37(a) kinasema “ikiwa suala lililochapishwa ni ukweli, basi si kashfa”, naomba nikushirikishe, msomaji. Mfano sisi Kampuni ya Jamhuri Media Limited, mwaka 2011 tulichapisha matangazo ya Wizara ya Kilimo. Tukawapa risiti ya EFD. Leo ni mwaka 2026, yaani miaka 15 baadaye, Wizara ya Kilimo haijawahi kutulipa.
Niulize TRA walituvumilia? Mwaka 2018 na mwaka 2019 walikamata akaunti zetu za kampuni, wakatoa kila senti iliyokuwamo wakabakiza fedha za kitabu Sh 100,000 kutokana na kodi za aina hii. Hawakujali kama tulikuwa na jukumu la kuchapisha gazeti, kumlipa mchapishaji (kiwanda), kulipa mishahara wafanyakazi au yeyote awaye. Ninapoandika haya, sisimuliwi yamenikuta. Hadi leo tunadai taasisi mbalimbali karibu Sh milioni 700, lakini kodi ya Sh milioni 5 inanitoa jasho. Mishahara na uchapaji wa gazeti nalala macho wazi kama ndege akiwa juu ya mti. Fedha hizi sisi tumeishazilipia kodi.
Jambo moja nikiri. Baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuingia madarakani Machi 19, 2021, haya manyanyaso kwa kiasi kikubwa yamekwenda likizo. Namshukuru Rais Samia, kwani naamini hotuba ya mwisho ya Waziri wa Fedha, ambaye sasa ni Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Lameck Nchemba, bungeni mwaka jana kuwa TRA wasifunge biashara bila kibali cha wazi kwa sababu ya kodi, imefanya kazi.
Sitanii, namshukuru Kamishna Mkuu wa TRA, Yusufu Mwenda, kwani tangu ameingia madarakani hadithi za kufungiwa akaunti zimemoka. Meseji za kutoka TRA zinazosomeka: “Lipa kodi kwa wakati kuepuka usumbufu na faini,” zimepungua. Kumbe nao wanajijua kuwa ni wasumbufu! Hata kampuni ile ya bia iliyokuwa imepigwa kufuli ikayumba, akaunti zake chini ya Kamishna Mkuu Mwenda zimefunguliwa. Wakati nikishukuru angalau hili la kutofunga akaunti, sisi tunaofanya biashara tumejawa na msongo wa mawazo.

Kwanza, lazima kuwe na utambuzi sahihi wa walipakodi wapya. Wale ambao hawapo kwenye mfumo kabisa. Kwa kutumia mifumo ya kidijitali—malipo ya simu, usajili wa biashara mtandaoni—serikali inaweza kuibua maelfu ya walipakodi wapya bila kuwanyanyasa. Pili, elimu ya kodi iongezwe. Watu wengi hawalipi si kwa ukaidi, bali kwa kutoelewa wajibu wao au kuona hakuna manufaa ya moja kwa moja.
Tatu, kodi zenye kero kubwa na wakati gani unalipa vipitiwe upya. Kodi zinazokandamiza uzalishaji au biashara ndogo ndizo ziwe za kwanza kuondolewa au kupunguzwa. Utaratibu wa kutoa EFD kabla ya kupokea malipo usitishwe au wapokea EFD wabanwe kulipa. Badala ya kukusanya kingi kutoka kwa wachache waliokata tamaa, ni bora kukusanya kidogo kutoka kwa wengi walio tayari kushiriki. Katika wingi wao, kitakuwa kingi. Elimu kwa mlipakodi kupitia vyombo vya habari ni muhimu kweli.
Nne, uwajibikaji wa matumizi ya kodi uonekane. Wananchi wakiona kodi zao zinajenga barabara, kuboresha afya na elimu, utii utaongezeka. Lakini kodi zikibaki kuwa mzigo usioonekana matokeo yake, zitaendelea kuchukiza. Hapa ndipo maafisa habari wa serikali wanapaswa kutangaza kwa kina kazi zinazofanywa na serikali bila kusubiri kuulizwa.
Sitanii, serikali inapaswa kubadili mtazamo kutoka kukusanya kodi kwa nguvu kwenda kujenga utamaduni wa ulipaji kodi kwa hiari – daktari na mgonjwa. Hii ni safari ya kuaminiana. Bila kupanua wigo wa walipakodi na kupunguza mzigo kwa wachache waliopo, hata mapendekezo 284 hayatafua dafu. Mfumo bora wa kodi si ule unaokusanya zaidi leo, bali ule unaojenga uendelevu wa kesho.
Kampeni ya “Ukinunua dai risiti, ukiuza toa risiti,” iongezewe kaulimbiu kuwa “Ukipewa risiti, toa malipo.” Sisi tuliotoa risiti ya EFD mwaka 2011, leo ni mwaka 2026, yaani miaka 15 baadaye, hadi leo hatujalipwa. Hasara halisi na hasara ya matarajio haielezeki. TRA kama ilivyopendekezwa iitwe Mamlaka ya Huduma, naunga mkono hoja. Wahamasishe pia watoa huduma kufanya malipo wakipewa EFD badala ya kuzipokea ‘wakameza pini’. Wafanyabiashara tuna maumivu ya kodi. Tuokoeni. Mungu ibariki Tanzania.

0784 404 827