Na Aziza Nangwa, Jamhuri Media, Dar es Salaam

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Jumanne Muliro, amewataka askari polisi kutekeleza majukumu yao ya msingi ya kusimamia sheria na kudumisha usalama wa raia.

Akizungumza katika eneo la Raha Square, Kariakoo wilayani Ilala baada ya kukutana na wafanyabiashara wa soko hilo,

Muliro amesema lengo la ziara hiyo lilikuwa kufuatilia masuala mbalimbali ya usalama pamoja na kusikiliza kero za wadau wanaofanya shughuli zao katika eneo hilo.

Amesema moja ya kero kubwa iliyowasilishwa na wafanyabiashara hao ni baadhi ya askari polisi, kuwakamata wafanyabiashara katika makutano ya barabara zinazoingia sokoni na kuwatuhumu kukosa vibali kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), hali inayosababisha usumbufu wakati wa kuingiza mizigo sokoni.

“Nimetoa maagizo kwa Kamanda wa Polisi Ilala kuhakikisha askari wanajikita katika majukumu yao ya msingi badala ya kufanya kazi zisizo zao.

“Kama kuna taarifa za uvunjifu wa sheria, polisi wanapaswa kuhoji na kushirikiana na mamlaka husika kama Uhamiaji, TRA au TBS badala ya kuchukua hatua binafsi,” amesema

Aliongeza kuwa baadhi ya askari wanaojihusisha na vitendo hivyo hawana nia njema kwani taratibu zingefuatwa kwa kuwashirikisha wakuu wao wa kazi badala ya kufanya mambo kwa maslahi binafsi, akisisitiza kuwa vitendo hivyo vinachafua taswira ya Jeshi la Polisi.

Muliro aliwapongeza wafanyabiashara wa Kariakoo kwa kuthamini ushirikiano wao na Jeshi la Polisi, akisema mchango wao umesaidia kuimarisha usalama wa eneo hilo.

Aidha, aliwapongeza watu binafsi walioweka kamera za ulinzi (CCTV) katika mitaa ya Kariakoo, akieleza kuwa teknolojia hiyo imesaidia kwa kiasi kikubwa kubaini wahalifu.

“Soko la Kariakoo kulikuwa na wizi wa mifukoni na kwenye magari, lakini kupitia kamera hizo tumefanikiwa kuwabaini wahusika mara moja,” amesema.

Amedai mikakati ya kuimarisha usalama ipo ya wazi na isiyo wazi, mradi tu inalenga kulinda maisha na mali za wananchi.

Pia alionya juu ya vyombo vya usafiri kama bajaji na maguta kufanya kazi kama daladala kwenye barabara kuu (highway), akisema hali hiyo ni hatari na inaweza kusababisha ajali.

“Sisi kazi yetu ni kulinda maisha ya watu na kusimamia sheria kwa kuzingatia utu na misingi ya kikatiba,” alisisitiza.

Muliro amesema Soko la Kariakoo ni kitovu cha biashara kinachokusanya watu wa mataifa mbalimbali, hivyo linahitaji ulinzi wa kuimarishwa ili kuweka mazingira salama ya kiuchumi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Soko la Kariakoo, Severin Mushi, amesema kamanda huyo amekuwa akifanya ziara za mara kwa mara eneo hilo lakini ombi lao ni kufanyiwa kazi kwa changamoto ya baadhi ya askari kuwazuia wanapoingiza mizigo.

Amesema askari hao husimama katika makutano ya barabara za Msimbazi na Karume na kuwazuia wafanyabiashara kana kwamba wao ni maofisa wa TRA au TBS.

“Wakati mwingine hata tukionyesha vibali halali, tunaambiwa havitoshi na tunaamriwa kusubiri,” amesema.

Aliongeza kuwa kero hiyo imesababisha baadhi ya wafanyabiashara wa kigeni kuhama na kwenda kufanya biashara katika maeneo mengine.

Hata hivyo, amesema wana matumaini kuwa maagizo ya Kamanda Muliro yatamaliza changamoto hiyo na kuwezesha wafanyabiashara kufanya shughuli zao kwa uhuru zaidi.