*Waziri Nanauka apewa Maua yake

*Mali Hai waiheshimisha Muheza

Na Byarugaba Innocent,ORMV

Ni takribani umbali wa kilometa 510 kwa mwendo wa gari Km 80 kwa saa unafikisha saa 11 njiani kutoka Dodoma Makao Makuu ya Serikali kufika Tanga.Ni safari iliyopambwa na hali ya hewa murua inayotokana na vichaka vifupi na uoto wa asili wenye miti minene ya Mibuyu,Miembe ikipambwa na Minazi mirefu inayoashiria Mazingira ya Kipwani.Tanga kunani jamani!

Ni ziara ya Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii inayoongozwa na Mhe.Hawa Mchafu Chakoma kukitembelea Kikundi cha vijana watano cha Mali Hai chenye usajili Na.184144 kilichopo Kata ya Genge, Wilaya ya Muheza kinachojishughulisha na Kazi ya utengenezaji wa bidhaa za Saruji.

Taarifa ya Kikundi inayosomwa na Clara Godfrey inatoa faraja kwa Wahe. Wabunge, inawatakafarisha mamia ya wananchi waliokuwepo.Haiwezekani bana!Haya ni masihara na usanii!Kutoka mtaji wa 100,000/-tena kwa kuchangishana mpaka kufikia Milioni 52!haiwezekani, alisikika Jafari Mhina akizungumza na Kibwana Shomari.

Godfrey amesema kuwa Kikundi cha Mali Hai kilianza Mwaka 2018 kikiwa na mtaji wa Shilingi 100,000.00 za kuchangishana kabla ya kukopeshwa Milioni 5 na Halmashauri kutoka kwenye asilimia 10 ya Mapato ya ndani kupitia asilimia 4 za Vijana.

Aidha,baada ya kuonesha uaminifu kwenye marejesho 2021/2022 Mali hai kiliongezwa mkopo kutoka kwenye mfuko wa Maendeleo ya Vijana (YDF) zilizotumika kununua vifaa mbalimbali,kuweka Umeme na kununua mashine za ‘perving blocks’ na zinazotengeneza Kalvati zenye kipenyo cha Diameter 90 kwa 60 zinazotumika kwenye Ujenzi wa barabara

Mafanikio yanabainishwa na Mwenyekiti wa Kikundi Timotheo Martin kuwa ni kuongezeka kwa mtaji kutoka 100,000-52,000,000 kutoa ajira kwa Vijana 20,Wanakukindi kuweza Kujenga makazi Yao,Kusomesha na kuhudumia familia pamoja na kuwa na Miradi mbadala.

Martin anabainisha Changamoto kuwa ni ukosefu wa gari kubwa la kubebea bidhaa zao,eneo dogo na kuwa na wateja wanaochelewa kulipa baada ya kuchukua bidhaa.Hata hivyo, Changamoto hizo zinatatuliwa uwandani na Mwenyekiti wa Kamati Mhe.Chakoma kwa kutoa Maelekezo kwa Wizara yenye dhamana na Mkoa wa Tanga kushughulikia na kupewa ufumbuzi hapo hapo hali inayoongeza tabasamu kwa Vijana wa Mali hai.

Pongezi zinamwagwa kwa Mhe.Joel Arthur Nanauka Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana kwa kuyaishi maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan kuendelea kuwajenga Vijana kutimiza ndoto zao kwa kuwawezesha kimitaji kupitia mfuko wa Vijana na kutoa rai kwa Vijana kuwa waaminifu kurejesha mikopo kwa wakati ili wanufaike wengi.

Mhe.Nanauka kwa unyenyekevu, furaha, tabasamu linaloashiria Upendo kwa vijana hasa wanatumia fursa zilizopo kutimiza ndoto zao anakiri kupokea maoni ya Kamati huku Changamoto zilizowalishwa na Vijana kuanza utekelezaji wake kwa vitendo.

Awali Mkuu wa Tanga Mhe.Balozi Batilda Burian anatoa takwimu kuwa Mkoa una Vijana 826,529 ambayo ni asilimia 31.6 ya idadi ya watu 2,615,597 wanaojishughulisha na ujasiliamali,kilimo,Ufugaji,bodoboda,usindikaji bidhaa na shughuli nyinginezo za kiuchumi.

Hata hivyo amebainisha kuwa katika kuunga mkono Maono ya Rais Samia kwa Mwaka wa fedha 2024/2025 Vikundi vya Vijana 1750 wamekopeshwa kiasi cha Shilingi bilioni 3.9 na kunufaisha Vijana 8,750

Wizara ya Maendeleo ya Vijana itaendelea kuwashirikisha Vijana wote nchini kwa kuvumbua fursa zinazopatikana na kutoa mitaji kuzitekeleza ili kila Kijana awe sehemu ya Kujenga uchumi wa Taifa…anasema Joel Arthur Nanauka Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana.