Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia, Dodoma
Wakati Watanzania wakiendelea kukumbwa na wimbi la kupanda kwa bei ya mafuta linalochochea gharama za maisha, Chama cha Mapinduzi (CCM) kimetoa maagizo matano mahsusi kwa Serikali yakilenga kudhibiti hali hiyo na kulinda uchumi wa Taifa.
Akizungumza leo Aprili 7,2026 Jijini Dodoma, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenan Kihongosi, amesema ongezeko hilo lina athari kubwa kwa wananchi na sekta mbalimbali za uchumi, hivyo hatua za haraka na za kimkakati ni muhimu zaidi kwa sasa.
Kihongosi ametaja miongoni mwa maagizo hayo ikiwemo kuanzishwa kwa mfuko maalum wa kuhimili mabadiliko ya bei za mafuta, ambao umefikia hatua za mwisho za maandalizi, ukiwa na lengo la kupunguza mshtuko wa bei kwa watumiaji.
Aidha ameielekeza Serikali kuendelea kuimarisha hifadhi ya mafuta ya kimkakati ili kuhakikisha upatikanaji wake unakuwa wa uhakika wakati wote, hususan katika nyakati za changamoto za soko la dunia.
Pia amesisitiza umuhimu wa kuimarisha miundombinu ya kuhifadhi mafuta ikiwemo ujenzi wa kituo kikubwa Kigamboni, kitakachosaidia kupunguza gharama za uingizaji na usambazaji wa bidhaa hiyo muhimu.
Chama hicho pia kimependekeza kuanzishwa kwa mfumo wa pamoja wa upokeaji mafuta katika ghala moja, hatua inayolenga kuondoa ucheleweshaji pamoja na kudhibiti udanganyifu unaoweza kujitokeza katika mchakato wa uingizaji.
Sambamba na hilo,ameshauri serikali kuimarisha uwezo wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) ili liweze kununua mafuta moja kwa moja bila kupitia kwa madalali, hatua itakayopunguza gharama zisizo za lazima.
Katika kupunguza utegemezi wa mafuta, amehimiza uwekezaji mkubwa katika usafiri wa umma na matumizi ya nishati mbadala kama gesi asilia, hususan kwa magari ya Serikali, bodaboda na bajaji.
Kihongosi amebainisha kuwa changamoto ya kupanda kwa bei ya mafuta si ya Tanzania pekee bali ni ya kimataifa, ikichangiwa na mabadiliko ya soko la dunia pamoja na migogoro ya kisiasa ikiwemo vita kati ya Urusi na Ukraine na mivutano ya Mashariki ya Kati.
Ameongeza kuwa Serikali imewahi kuchukua hatua za kupunguza makali ya hali hiyo, ikiwemo kutoa ruzuku ya zaidi ya shilingi bilioni 100 mwaka 2022, na kwamba hatua kama hizo zinaweza kuendelea kuchukuliwa kulingana na mahitaji.
Katika hatua nyingine, Kihongosi amemtaka Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, John Heche, kuacha upotoshaji katika kauli zake na kusisitiza umuhimu wa kuzungumza kwa uhalisia.
Aidha, amegusia suala la uhuru wa kutoa maoni akibainisha kuwa uhuru huo haupaswi kuchanganywa na matumizi ya lugha ya matusi, huku akisisitiza kuwa mijadala ya kitaifa inapaswa kufanyika kwa heshima, ukweli na kwa kuzingatia maslahi ya Taifa.



