Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro Bw. Abdul-Razaq Badru leo tarehe 9 Aprili, 2026 amepuliza rasmi Kipenga cha shindano la mwezi mmoja la Safari Field Challenge akisisitiza kwamba Ngorongoro ni nyumbani kwa kila binadamu kutokana na chimbuko la historia linalobainishwa kisayansi.

Akizindua shindano hilo Kamishna Badru amewashukuru washiriki nane (8) wa shindano hilo kwa kuitika wito wa Ngorongoro na kuwaeleza kuwa Hifadhi ya Ngorongoro ni zaidi ya Kreta hasa kutokana na kuwa na utamaduni, asili, chimbuko la binadamu wa kale, siri ya Binadamu na maisha yake, Nyayo za Laetoli zenye umri za zaidi ya miaka milioni 3.6, mchanga unaohama, kushuhudia pumzi ya kwanza ya Nyumbu eneo la Ndutu, kuona Wanyama wakubwa watano katika eneo moja, mlima Lolmalasian ambao wa tatu kwa urefu Tanzania, misitu, mimea na ndege mbalimbali.

“Karibuni Ngorongoro ambapo ni nyumbani kwa sisi sote, mtapata uzoefu ya maajabu mbalimbali, kuyahisi, kuyaishi, kufurahia, kuyahadithia na kuwasaidia kupata ujuzi ambao utawafanya muwe mabalozi wazuri kuwaelezea watu wengine mkusanyiko wa maajabu yaliyoko Ngorongoro” Alisema Kamishna Badu.

Kamishna Badru amewapa changamoto washiriki wa shindano hilo kuwa watundu wa kuifahamu Ngorongoro, kuisemea Ngorongoro kwa mtazamo mpya wa sauti moja ambapo kwa kushirikiana na Azam Media hadithi, historia, maajabu ya Ngorongoro itasimuliwa na kufika pembe nne za dunia kuwa Ngorongoro sio kivutio cha utalii pakee bali ni Nyumbani kwa kila Binadamu ambapo historia yao ilianza.

Kamishna Msaidizi Mwandamizi anayesimamia Huduma za Utalii na masoko Mariam Chuma Kobelo amewaeleza washiriki wa Safari Field Challenge kuwa Tanzania ina vitu vingi za Kujivunia lakini Ngorongoro kuna vingi zaidi na kuwasisitiza washiriki wa shindano hilo kwenda kujifunza, kuifahamu na kuisimulia Ngorongoro kuwa ni zaidi ya Kasoko ya Ngorongoro.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tanzania Tour Guide Fondation (TTGF) Mosses Njole ameleza kuwa washiriki wote 8 wako timamu na wamejiandaa kikamilifu kushiriki shindano hilo na kuwapongeza Ngorongoro kwa kuwa wadhamini wakuu na wadau wengine wakiwepo Azam Media ambayo imekuwa sehemu ya kusimulia maajabu ya Ngorongoro.