Na Dotto Kwilasa, Dodoma
WAZIRI wa Afya, Mohamed Mchengerwa, ametoa maelekezo mapya kwa watoa huduma za afya nchini kuhakikisha kila mgonjwa anayefika hospitalini anapatiwa elimu kuhusu umuhimu wa kujiunga na Bima ya Afya, huku akitaka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kuboresha mifumo yake ya kidijitali ili kurahisisha upatikanaji wa vitambulisho kwa wananchi.
Maelekezo hayo yametolewa Novemba 29, 2026, wakati wa mbio za NHIF Marathon 2026 zilizofanyika katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 25 ya kuanzishwa kwa mfuko huo, ambapo Serikali imeeleza dhamira ya kuongeza wigo wa wananchi wanaopata huduma za afya kupitia mifumo ya bima.
Mchengerwa amesema kila mgonjwa anayefika katika kituo cha kutolea huduma za afya, baada ya kupatiwa huduma kwa kufuata taratibu za kitaalamu, anapaswa kuulizwa kama ana kitambulisho cha bima ya afya na wale wasio nacho waelimishwe umuhimu wa kujiunga ili kujihakikishia huduma za matibabu wanapozihitaji.
Amesisitiza kuwa NHIF inapaswa kuimarisha mifumo yake ya kidijitali ili wananchi waweze kupata vitambulisho vya bima kwa urahisi na kwa wakati, sambamba na kujenga imani kwa wanachama kwa kuhakikisha madai ya fidia kwa vituo vya kutolea huduma za afya yanalipwa kwa wakati.
Akizungumzia umuhimu wa kinga dhidi ya magonjwa, Mchengerwa amesema magonjwa yasiyoambukiza yanachangia zaidi ya asilimia 37 ya matumizi ya NHIF, hivyo amewataka Watanzania kufanya mazoezi mara kwa mara na kupima afya zao ili kubaini mapema vihatarishi vya magonjwa kama kisukari, saratani na magonjwa ya moyo.
Amesema taifa lenye wananchi wenye afya njema lina nafasi kubwa ya kuimarisha maendeleo yake, akiwataka mameneja wa NHIF katika mikoa yote kuendeleza hamasa ya mazoezi na kuelimisha wananchi kuhusu faida za bima ya afya ili kupunguza mzigo wa gharama za matibabu kwa familia na Serikali.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, amewataka Watanzania kujiunga na mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, akisema hatua hiyo itasaidia wananchi kupata huduma za afya kwa wakati na kupunguza gharama za matibabu zinazobebwa na familia na Serikali.
Dkt. Samizi amesema maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni kujenga taifa lenye afya njema kwa kuwekeza katika kinga dhidi ya magonjwa badala ya kusubiri wananchi waumwe, hatua itakayosaidia kupunguza gharama za matibabu na kuelekeza rasilimali katika shughuli nyingine za maendeleo.
Amesema kupitia awamu ya kwanza ya mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, Serikali ililipia kaya 276,000 zisizo na uwezo kwa gharama ya Sh bilioni 48, ambapo asilimia 90 ya kaya hizo zimeanza kunufaika na huduma za afya, hususan katika vituo vya huduma za afya ya msingi.
Ameeleza kuwa awamu ya pili iliyozinduliwa Oktoba 22, 2026, mkoani Mtwara, inalenga kusajili kaya nyingine 625,000, na kufanya jumla ya kaya zitakazolipiwa na Serikali kufikia 901,000 kwa gharama ya zaidi ya Sh bilioni 98.
Aidha, amewahimiza wananchi wenye uwezo kujiunga na mpango huo kupitia kifurushi cha Bahari cha Sh 150,000 kwa mwaka, kinachotoa huduma 370 za afya kwa kaya yenye watu sita, sawa na Sh 25,000 kwa kila mtu kwa mwaka.
Akizungumzia kampeni ya Zijue Namba Zako iliyozinduliwa na Waziri wa Afya, Dkt. Samizi amesema wananchi wanapaswa kufahamu hali ya afya zao kwa kupima viashiria muhimu, ikiwemo shinikizo la damu, kiwango cha sukari na mafuta mwilini pamoja na afya ya figo, ili kubaini mapema vihatarishi vya magonjwa yasiyoambukiza.
Amesema asilimia 61 ya mapato ya NHIF yanatumika kuhudumia wagonjwa wa magonjwa yasiyoambukiza, hivyo amesisitiza umuhimu wa kufanya mazoezi, kula chakula bora, kupunguza matumizi ya pombe, kuepuka uvutaji sigara na kupima afya angalau mara moja kwa mwaka.
Dkt. Samizi amempongeza Waziri Mchengerwa kwa juhudi za kusimamia sekta ya afya, akibainisha kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora za afya kwa wakati, kwa gharama nafuu na kwa usawa.




