Na Joseph Mahumi, WF, Dar es Salaam
Serikali imesema itaendelea kuimarisha usimamizi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuhakikisha rasilimali zinazotolewa na washirika wa maendeleo zinatumika kwa ufanisi na kuleta manufaa yanayokusudiwa kwa wananchi.
Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, wakati wa ufunguzi wa Kikao cha Mapitio ya Utendaji wa Miradi ya Maendeleo ya Serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia kwa mwaka 2026 (Country Portfolio Performance Review – CPPR), kilicholenga kutathmini utendaji wa miradi inayoendelea, kubaini changamoto za utekelezaji na kukubaliana hatua za vitendo za kuongeza ufanisi wa fedha za maendeleo, kilichofanyika Benki Kuu ya Tanzania, jijini Dar es Salaam.
Dkt. Mwamba alisema kuwa mafanikio ya miradi ya maendeleo hayapaswi kupimwa kwa kiasi cha fedha kilichopatikana, mikataba ya ufadhili iliyosainiwa au fedha zilizotolewa, bali kwa matokeo halisi na endelevu yanayoboresha maisha ya wananchi.
“ufadhili wa miradi ni nyenzo ya kufikia maendeleo na si lengo lenyewe, hivyo mafanikio yanapaswa kuonekana kupitia miundombinu iliyokamilika, huduma bora za umma, fursa zaidi za kiuchumi na kuboreka kwa maisha ya wananchi” alisema Dkt. Mwamba
Alisema msisitizo huo unaendana na hatua ya Tanzania kuanza kutekeleza Dira 2050, inayoungwa mkono na Mpango wa Muda Mrefu wa Maendeleo pamoja na Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP IV), ambayo inalenga kujenga uchumi shindani, jumuishi, himilivu na wenye ustawi.
Katika kufikia malengo hayo, alisema Benki ya Dunia imeendelea kuwa mshirika muhimu wa kimkakati wa Tanzania kwa kutoa ufadhili na utaalamu katika sekta mbalimbali zikiwemo uchukuzi, nishati, kilimo, elimu, afya, maji, maendeleo ya mijini na ulinzi wa jamii.
Hata hivyo, Dkt. Mwamba alieleza kuwa pamoja na umuhimu wa rasilimali hizo, bado kuna haja ya kuimarisha ufanisi katika maandalizi na utekelezaji wa miradi ili kuondoa vikwazo vinavyochelewesha upatikanaji wa matokeo yaliyokusudiwa.
Alibainisha kuwa Serikali imechukua hatua mbalimbali za kitaasisi na kiutawala kukabiliana na changamoto hizo, zikiwemo kuanzishwa kwa Mwongozo wa Kitaifa wa Uidhinishaji wa Miradi ya Maendeleo (National Development Projects Approval Guideline-NDPAG), kuboresha mifumo ya manunuzi ya umma na usimamizi wa fedha, pamoja na kuendelea kuimarisha usimamizi wa vihatarishi vya kimazingira na kijamii.
“Serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na Benki ya Dunia katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto zilizopo, akibainisha kuwa mafanikio ya ushirikiano huo yanategemea uwajibikaji wa pande zote, maamuzi ya wakati na dhamira ya pamoja ya kufikia malengo ya maendeleo” alisema Dkt. Mwamba
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Bw. Firas Raad, alisema Benki hiyo itaendelea kuwa mdau muhimu wa Maendeleo nchini Tanzania ili kuhakikisha malengo ya Dira 2050 yanafikiwa.
Alisema kuwa thamani ya majadiliano ya kikao hicho yatasaidia utekelezaji mzuri wa miradi na kuleta mabadiliko chanya katika maisha ya wananchi.
Kikao hicho cha CPPR kiliwakutanisha viongozi na wataalamu kutoka Serikalini na Benki ya Dunia kwa lengo la kutathmini utendaji wa miradi inayoendelea, kubaini changamoto za utekelezaji na kukubaliana hatua za vitendo za kuongeza ufanisi wa fedha za maendeleo.









