Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Amos James Ibrahim, akipokelewa na baadhi ya watumishi wa Wizara ya Fedha, alipowasili katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam, mara baada ya kuaminiwa na kuapishwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ikulu, jijini humo.

******************

Na. Joseph Mahumi, WF, Dar es Salaam

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), ameongoza viongozi pamoja na watumishi wa Wizara ya Fedha kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) kumkaribisha Naibu Katibu Mkuu mpya anayesimamia masuala ya Uchumi, Dkt. Amos James Ibrahim, katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha jijini Dar es Salaam, mara baada ya kuaminiwa na kuapishwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika nafasi hiyo.

Katika mapokezi hayo, Mhe. Munde alimweleza matarajio ya Wizara katika kuimarisha usimamizi wa uchumi, kuongeza kasi ya utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya Taifa, na kusisitiza umuhimu wa ushirikiano, weledi, ubunifu na kuweka malengo yanayopimika katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara, ili kuwezesha Tanzania kufikia dhamira yake ya uchumi wa dola za Marekani trilioni moja ifikapo mwaka 2050.

Aidha, Mhe. Munde alimhakikishia Dkt. Amos James Ibrahim, ushirikiano wa viongozi na watumishi wa Wizara, akieleza kuwa uzoefu, weledi na mshikamano wa watumishi ni msingi muhimu katika kuimarisha utendaji na kufanikisha majukumu ya Wizara ya Fedha.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Amos Ibrahim alishukuru kwa mapokezi na nafasi aliyopewa, akieleza dhamira yake ya kuungana na timu iliyopo, kujifunza kutoka kwa watumishi wenye uzoefu na kushirikiana katika kutekeleza majukumu ya Wizara kwa ufanisi.

Dkt. Ibrahim alisisitiza umuhimu wa kuzingatia misemo ya “Kazi Iendelee” na “Kazi na Utu,” kwa kuwa utekelezaji wa majukumu unapaswa kuambatana na ushirikiano, kuheshimiana, kuthaminiana na kutumia maarifa na uzoefu wa watumishi katika kufanya maamuzi yenye tija.

Aliongeza kuwa katika dunia inayobadilika kwa kasi, ikiwemo matumizi ya teknolojia na Akili Unde (AI), ni muhimu taasisi kuendelea kujifunza, kuwa wazi kwa mawazo mapya na kutumia rasilimali watu waliopo ili kuimarisha utendaji na kutoa mchango katika maendeleo ya Taifa.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha anayesimamia masuala ya Uchumi, Dkt. Amos James Ibrahim (Kushoto), akilakiwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha anayesimamia Huduma za Hazina, Bw. Nsubili Joshua na baadhi ya watumishi wa Wizara ya Fedha, alipowasili katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam, mara baada ya kuaminiwa na kuapishwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ikulu, jijini humo.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha anayesimamia masuala ya Uchumi, Dkt. Amos James Ibrahim (Kushoto), akizungumza jambo wakati wa kikao chake cha mapokezi kilichoongozwa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (hayupo pichani) katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam, mara baada ya kuaminiwa na kuapishwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ikulu, jijini humo.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Dar es Salaam)