NA; MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

Tanzania imepata ahadi na fursa za uwekezaji zenye thamani ya takribani dola za Marekani bilioni 4.7 kupitia Mkutano wa 31 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP31), uliofanyika Antalya, Uturuki.

Fedha hizo zinatarajiwa kuelekezwa katika miradi mbalimbali ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo nishati safi ya kupikia, nishati jadidifu, uhifadhi wa mifumo ya ikolojia, ulinzi wa jamii zilizo katika hatari ya athari za tabianchi pamoja na kuimarisha uchumi wa kijani.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio yaliyopatikana kutokana na ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo uliofanyika kuanzia Novemba 09 hadi 20, 2026.

Alieleza kuwa ushiriki wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mkutano huo ulikuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha nafasi ya Tanzania kimataifa na kufungua fursa mbalimbali za ushirikiano na uwekezaji.

Aidha, Masauni alisema Rais Samia katika hotuba yake aliyotoa Novemba 11, 2026 alisisitiza vipaumbele vitatu ambavyo ni upatikanaji wa fedha za kutosha na zenye masharti nafuu za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kuimarisha mpito wa haki wa nishati na kuendeleza maendeleo jumuishi kupitia teknolojia, ubunifu na ajira za kijani kwa kuzingatia Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050.

Akizungumzia mafanikio katika eneo la fedha, Masauni alisema Benki ya Maendeleo ya Afrika imeidhinisha ufadhili wa ununuzi wa majiko 70,000 ya kisasa yanayotumia umeme kwa ajili ya shule na vituo vya afya, yenye thamani ya dola milioni 54.

Alisema kuwa majiko mengine 70,000 yenye thamani sawa na hiyo yanatarajiwa kuidhinishwa kupitia mradi mwingine wa nishati unaofadhiliwa na benki hiyo.

Aidha, taasisi ya Sustainable Energy for All (SEforALL) imeahidi kuijumuisha Tanzania katika mpango wa uwekezaji unaozidi dola bilioni nne kwa ajili ya kuimarisha matumizi ya nishati safi ya kupikia na kusaidia nchi kuwa kitovu cha uzalishaji wa majiko na teknolojia husika.

Alisema Serikali ya Uingereza kupitia UK Aid imeahidi pauni milioni mbili, sawa na dola milioni 2.6, kwa ajili ya nishati safi ya kupikia na pauni nyingine milioni mbili kwa nishati jadidifu.

Kupitia mpango huo, wananchi milioni moja wanatarajiwa kunufaika kwa kupata majiko ya umeme na kulipia gharama zake kidogo kidogo kupitia bili za umeme.

Masauni aliongeza kuwa mfuko wa Green Climate Fund (GCF) umeahidi dola milioni sita kwa ajili ya kuimarisha uwezo wa nchi kuandaa na kutekeleza miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Alisema Tanzania pia imepata mafanikio baada ya Baraza la Taifa la Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira (NEMC) kupata ithibati ya GCF, hatua inayoiwezesha taasisi hiyo kupata fedha za moja kwa moja kwa ajili ya miradi ya mazingira.

Alisema kwa sasa Tanzania ina taasisi mbili zenye ithibati ya mfuko huo ambazo ni NEMC na Benki ya CRDB, huku Wizara ya Fedha ikiwa katika hatua za mwisho za kupata ithibati hiyo.

Mkutano wa COP31 ulikuwa na kaulimbiu ya kitaifa “Hatua Jumuishi za Tanzania za Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi kwa Ajili ya Dira ya 2050: Kujenga Taifa Imara la Kijani na Lenye Ustawi” ikilenga kusisitiza umuhimu wa kuhusisha makundi yote ya jamii katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kujenga ustahimilivu wa taifa, kuimarisha uchumi wa kijani na kuhakikisha ustawi wa wananchi.