Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo imeendelea kung’ara katika eneo la usimamizi wa fedha za umma baada ya kushika nafasi ya tatu katika Tuzo za Ubora wa Uandaaji na Uwasilishaji wa Taarifa za Fedha kwa mwaka 2025, zinazotolewa na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), katika kundi la majiji na manispaa.
Akizungumza katika hafla ya utoaji wa tuzo hizo mapma leo 26 November 2026 Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, CPA Prof. Siasa Mzenzi, alisema kuwa jumla ya washiriki 138 waliwasilisha taarifa za fedha kwa ajili ya kushindanishwa katika tuzo za mwaka 2025.
Alieleza kuwa tathmini ilifanyika kwa hatua mbili ambazo ni tathmini ya awali (Preliminary Evaluation) na tathmini ya kitaalamu (Technical Evaluation), kwa kuzingatia vigezo mbalimbali vya ubora wa taarifa za fedha.
Aidha Katika kueleza umuhimu wa tuzo hizo, NBAA imebainisha kuwa tuzo hizo zinalenga kutambua na kuhamasisha taasisi, majiji, manispaa na mashirika yanayofanya vizuri katika uandaaji na uwasilishaji wa taarifa za fedha kwa kuzingatia viwango vya kitaaluma, uwazi, usahihi na uwajibikaji pamoja na kuimarisha utamaduni wa usimamizi bora wa fedha na kuongeza ufanisi katika utoaji wa taarifa za kifedha kwa taasisi za umma na binafsi.
Prof. Mzenzi alisisitiza kuwa taasisi zinazopata tuzo hizo hazipaswi kuzichukulia kama mwisho wa safari, bali zinapaswa kuendelea kuboresha utendaji, kuimarisha mifumo ya usimamizi wa fedha na kudumisha ushindani katika viwango vya juu vya kitaaluma.
Nafasi hiyo ya tatu ni sehemu ya jitihada za Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo katika kuimarisha uwazi, uwajibikaji na usimamizi madhubuti wa rasilimali za umma.
Mafanikio hayo yanaendelea kuitangaza Manispaa ya Ubungo katika eneo la uandaaji na uwasilishaji bora wa taarifa za fedha, huku yakiwa chachu ya kuendeleza ubora na ufanisi katika usimamizi wa fedha kwa manufaa ya wananchi.


