Qingdao, China
Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera, amesisitiza umuhimu wa vijana kushiriki kikamilifu katika miradi ya nishati itakayotekelezwa kupitia ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP), akieleza kuwa miradi hiyo ni chanzo kikubwa cha ajira, ujuzi na ubunifu utakaoweza kuharakisha maendeleo ya uchumi.
Akizungumza katika Mkutano wa nne wa Mawaziri wa Nishati kwenye Kongamano la Vijana la Belt and Road Partnership lililofanyika Qingdao nchini China, Leo Novemba 25, 2026 Dkt. Homera amesema kuwa vijana ndio watakaokuwa nguzo kuu ya maendeleo ya sekta ya nishati katika siku zijazo kwani wao ndiyo watakaobuni, kuendesha na kuboresha mifumo ya nishati ya miongo ijayo.
Ameeleza kuwa Serikali ya Tanzania imeweka mazingira wezeshi ya kuvutia uwekezaji wa sekta binafsi katika nishati, ikilenga kukusanya takriban dola za Marekani bilioni 4.039 ifikapo mwaka 2030 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya uzalishaji na usambazaji wa nishati.
Ameitaja baadhi ya miradi ya kimkakati inayotarajiwa kutekelezwa kwa mfumo wa PPP kuwa ni pamoja na mitambo ya kuzalisha umeme kwa gesi ya Chalinze I na II, miradi ya upepo ya Singida na Makambako, miradi ya sola ya Kishapu na Kisima-Dodoma pamoja na miradi ya kuzalisha umeme wa maji ya Ruhudji, Rumakali na Kikonge.
Aidha, amesema utekelezaji wa miradi hiyo unahitaji wataalamu wengi vijana wenye ujuzi katika maeneo mbalimbali ikiwemo uhandisi wa umeme, jiolojia, mifumo ya usafirishaji wa umeme, uchambuzi wa data, ufadhili wa miradi na ufundi, huku akisisitiza kuwa ni wakati sahihi kwa vijana kujiandaa kunufaika na fursa hizo.
Katika hatua nyingine, Dkt. Homera amewaalika vijana wa China kushirikiana na vijana wa Kitanzania katika kuendeleza teknolojia na ubunifu utakaosaidia kutumia rasilimali za nishati zilizopo nchini kwa gharama nafuu na kwa tija zaidi.
Pia amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya vyuo vikuu, taasisi za utafiti na sekta binafsi katika kuimarisha mafunzo, tafiti na kubadilishana uzoefu kwa vijana, hatua ambayo itaongeza uwezo wao wa kushiriki kikamilifu katika mabadiliko ya nishati na uchumi wa kijani.
Ameeleza kwamba mafanikio ya sekta ya nishati yatategemea zaidi ushiriki wa vijana wenye maarifa, ubunifu na uwezo wa kuleta suluhisho endelevu katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayofanyika kupitia ushirikiano wa serikali na sekta binafsi.













