Na Pendo Nguka, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Tanzania kuwa kitovu cha nishati na usafirishaji katika ukanda wa Afrika Mashariki kupitia utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati iliyokubaliwa kati yake na Uganda, ikiwamo uendelezaji wa miundombinu ya nishati Tanga, reli ya kisasa (SGR) na kuimarisha usafiri wa majini katika Ziwa Victoria.

Hatua hiyo inatarajiwa kuongeza uwezo wa Bandari ya Dar es Salaam kuhudumia mizigo ya nchi jirani, kupanua biashara, kuvutia uwekezaji na kufungua fursa za ajira kwa vijana katika sekta mbalimbali.

Waziri wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa amesema hayo wakati akielezea mafanikio ya ziara ya kikazi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu nchini Uganda iliyofanyika Novemba 18 hadi 19 mwaka huu kwa mwaliko wa Rais wa nchi hiyo, Yoweri Museveni.

Amesema katika ziara hiyo viongozi hao walifanya mazungumzo yaliyowezesha kufikiwa kwa makubaliano muhimu yenye lengo la kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, hususan katika sekta za uchukuzi, nishati, biashara, uwekezaji na maendeleo ya viwanda.

Akifafanua maeneo yenye manufaa kwa Tanzania, Profesa Mbarawa amesema moja ya makubaliano muhimu ni kuharakisha mpango wa kuifanya Tanga kuwa kitovu cha nishati cha kikanda (Regional Energy Hub).

Anasema mpango huo utahusisha uendelezaji wa miundombinu ya kuhifadhi, kusafirisha na kusambaza mafuta pamoja na kuimarisha huduma za usafirishaji na ugavi.

Aidha, viongozi hao wamekubaliana kuendeleza ushirikiano katika uzalishaji wa mbolea, plastiki, kemikali za viwandani na bidhaa nyingine zinazotokana na mafuta.

Llengo ni kuhakikisha Tanzania hainufaiki kwa kupitisha mafuta pekee, bali inakuwa kitovu cha shughuli za kiuchumi zinazohusiana na nishati, viwanda na biashara.

Uwekezaji huo unatarajiwa kufungua ajira katika ujenzi, uhandisi, uendeshaji wa mitambo, usafirishaji, matengenezo ya vifaa na shughuli nyingine za viwandani, huku vijana wajasiriamali wakipata nafasi za kutoa huduma mbalimbali.

EACOP kufikia asilimia 93.9

Katika hatua nyingine, Profesa Mbarawa amesema viongozi hao walipokea taarifa ya maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), ambao umefikia asilimia 93.9 ya utekelezaji.

Amesema viongozi hao wameelekeza kazi zilizobaki kukamilishwa kwa haraka ili kuwezesha kuanza kwa usafirishaji wa mafuta.

Ameeleza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutafungua fursa katika uendeshaji, matengenezo, usalama, usafirishaji na huduma za ugavi (logistics), huku ukichochea uwekezaji na shughuli nyingine za kiuchumi katika maeneo yote yanayopitiwa na bomba hilo.

Mradi huo unatarajiwa kuleta mabadiliko ya kiuchumi katika ukanda mzima unaopitiwa na miundombinu hiyo.

Reli ya SGR kuunganisha Tanzania na Uganda

Akizungumzia eneo la tatu, amesema Tanzania na Uganda zimekubaliana kusaini mkataba wa mfumo wa ushirikiano (Framework Agreement) kwa ajili ya kuendeleza mradi wa reli ya kisasa katika njia ya Isaka–Lusahunga–Murongo–Kikagati–Mpondwe yenye urefu wa kilomita 620.

Mradi huo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha muunganiko wa reli kati ya nchi hizo mbili na kuongeza uwezo wa Bandari ya Dar es Salaam kuhudumia mizigo ya Uganda
.

Amebainisha kuwa kwa sasa Bandari ya Dar es Salaam husafirisha kiwango cha juu cha takribani tani 200,000 za mizigo ya Uganda, wakati nchi hiyo ina mahitaji ya takribani tani milioni 11.

Hali hiyo inatokana kwa kiasi kikubwa na upungufu wa miundombinu inayowezesha usafirishaji wa mizigo kwa kiwango kikubwa zaidi.

Aidha kukamilika kwa reli hiyo kutapunguza gharama na muda wa usafirishaji, kufungua uwekezaji katika vituo vya usafirishaji, maghala, huduma za ugavi na biashara, pamoja na kuchochea shughuli za kiuchumi katika maeneo itakayopita.

Amesema uzoefu wa reli ya SGR kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma umeonyesha namna miundombinu ya usafiri inavyoweza kuchochea mabadiliko ya kiuchumi katika maeneo husika.

Hata hivyo mradi huo bado unahitaji kukamilisha hatua za upembuzi yakinifu, usanifu wa kitaalamu na maandalizi ya upatikanaji wa fedha kabla ya kuanza ujenzi.

Baada ya kukamilika kwa upembuzi yakinifu, Serikali itaweza kubaini kwa kina njia itakayopitiwa na reli hiyo na kuanza hatua za kutafuta fedha kwa ajili ya utekelezaji wake..

Ziwa Victoria kufungua njia mpya za biashara

Katika eneo la nne, Profesa Mbarawa amesema viongozi hao wamekubaliana kuimarisha usafiri wa majini katika Ziwa Victoria kwa kuboresha miundombinu ya Bandari ya Port Bell nchini Uganda na kuimarisha muunganiko wake na reli.

Hatua hiyo itaiwezesha Tanzania kutumia vizuri miundombinu iliyopo ya usafirishaji wa mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam kupitia reli ya kati hadi Mwanza na kuendelea na usafirishaji kwa njia ya Ziwa Victoria.

Mpaka sasa tayari Tanzania ina miundombinu ya bandari katika Ziwa Victoria, hivyo kinachohitajika ni kuboresha upande wa Uganda, hususan Bandari ya Port Bell na reli inayounganisha eneo hilo na maeneo mengine.

Kukamilika kwa reli ya SGR kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma, Tabora, Isaka na Mwanza kutatoa fursa ya kusafirisha mizigo mingi zaidi kupitia Bandari ya Mwanza kuelekea Uganda.

Anasema kuimarika kwa njia hiyo kutasaidia kuongeza matumizi ya miundombinu ya uchukuzi, kupanua biashara na kuchochea shughuli za kiuchumi katika Kanda ya Ziwa.